Wananchi watoa malalamiko kwa Mkuu wa Mkoa kuhusu kubomolewa nyumba zao


Wamiliki wa viwanja eneo la Pasua ambako nyumba zaidi ya 70 zilizowekwa alama ya X na Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco) kwa ajili ya kubomolewa wamesema kuwa na hatimiliki halali zililzotolewa na mamlaka pamoja na kupatiwa vibali vya ujenzi

Wananchi hao wametowa malalamiko hayo baada ya Kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Kilimanjaro ikiongozwa na Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira kutembelea eneo hilo ambapo wamesema walipewa vibali pamoja na kutambulika kwa kuendelea kulipia viwanja vyao kodi ya majengo na ya pango.

Kwa mujibu wa wananchi hao waligawiwa eneo hilo na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kati ya mwaka 2005 na 2010 baada ya eneo hilo kubadilishwa matumizi na kuwa la makazi hivyo kutaka fidia kabla ya kubomolewa nyumba zao.

Wananchi hao wameeleza mwaka 1962 eneo hilo lenye viwanja 90 lilipendekezwa kupitishwa reli ambayo ingehudumia viwanda ambavyo hata hivyo havikujengwa ambapo mwaka 2002 halmashauri iliomba kubadili matumizi ya eneo ambalo lilipangwa kupita reli ombi linaloelezwa kuwa liliridhiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Hatua ya kamati hiyo kutembelea eneo hilo inakuja baada ya Wiki iliyopita mkuu wa mkoa, Bi. Mghwira kuagiza Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kukutana na Rahco ili kutatua mgogoro huo.

No comments: