Mh.Rais Magufuli ameagiza kujengwa ukuta kuzunguka mgodi wa Tanzanite Mirerani
Rais wa Tanzania John Magufuli ameliagiza Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kujenga ukuta wa kuzunguka vitalu vya kuanzia A hadi D vyenye madini ya Tanzanite katika eneo la Mererani, Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara ili kudhibiti uchimbaji na biashara ya madini hayo.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo kwenye sherehe ya ufunguzi wa barabara ya Kia - Mererani iliyofanyika katika eneo la Mererani.
Rais Magufuli amesema pamoja na kujenga ukuta huo haraka iwezekanavyo, soko la Tanzanite litapaswa kuwa katika eneo hilo, Tanzanite yote itapita kupitia lango moja na ameitaka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kushiriki katika ununuzi wa Tanzanite.
"Lile eneo la kitalu kuanzia A hadi D ambalo ndio lina mali nyingi ya Tanzanite, naagiza Jeshi la Wananchi kupitia Suma-JKT na wengine, najua wameshamaliza utafiti, waanze kujenga ukuta eneo hilo lote na kazi hii ifanyike haraka, watakapojenga ukuta wataweka kamera na patakuwa na mlango mmoja ambapo patajengwa vifaa maalum, nataka niwaeleze ukweli ndugu zangu wa Simanjiro hata kama utameza Tanzanite itaonekana" amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amevipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa hatua zilizoanza kuchukuliwa kukabiliana na wizi wa madini ya Tanzanite na ameitaka kamati inayoongozwa na Waziri wa Sheria na Katiba Prof. Palamagamba John Kabudi kuanza kufanyia kazi taarifa zilizotolewa na wananchi kuhusu uchimbaji na biashara ya madini hayo ili mchakato wa kurekebisha mikataba ufanyike.
"Ripoti ya kamati iliyoundwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai imeonesha kuwa Serikali na wananchi tunanufaika kwa asilimia 5 tu ya madini haya ya Tanzanite, zinazobaki zote wananufaika watu wengine, hii haiwezekani ni lazima tuwe na mikataba itakayotunufaisha na sisi, haiwezekani Tanzanite tunayo sisi tu lakini tunapata asilimia 5, halafu hapa Mererani hakuna maji na hakuna gari ya wagonjwa" amesisitiza Rais Magufuli.
Hata hivyo Rais Magufuli amewaahidi wananchi wa Mererani kuwa atawapelekea gari la wagonjwa na pia atalifanyia kazi tatizo la uhaba wa maji linalowakabili wananchi hao.
Mapema akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara ya Kia - Mererani yenye urefu wa kilometa 26, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa alisema ujenzi huo umegharimu Shilingi Bilioni 32 na kwamba barabara hiyo itaunganisha eneo la madini ya Tanzanite la Mererani na eneo la uwekezaji la Mererani, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na barabara kuu ya Moshi - Arusha.
No comments: