Rais Magufuli amaliza ziara kwa kupiga marufuku


Rais Dkt. John Magufuli amemaliza ziara yake katika Mkoa wa Arusha hii leo huku akisisitiza kwamba ni marufuku kwa mfanyakazi yeyote kuhamishwa katika kituo chake cha kazi pasipo kulipwa stahiki zake.

Rais Magufuli amesema hayo wakati alipokuwa yupo njiani kuelekea uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ambapo alisimamishwa na wananchi wa Sangsi nje kidogo ya Jiji la Arusha na wananchi wa Pacha ya Kia Mkoani Kilimanjaro na kuwahakikishia kuwa serikali itaendelea kutatua kero za wananchi na kuwahudumia bila kuwabagua kwa misingi ya itikadi za kisiasa, dini na ukabila.

Mhe. Rais Magufuli amesema katika kutimiza azma hiyo serikali inatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara ya Usa River  – Arusha inayojengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 139, mradi wa maji wa Arusha utakaogharimu Shilingi Bilioni 42, mradi wa kusambaza umeme katika vijiji zaidi ya 200 na mingine mingi inayotekelezwa katika maeneo hayo.

“Nina uhakika nyinyi wakazi wa Arusha mnaona Arusha inavyobadilika, kabla ya kujengwa barabara hii kulikuwa kunatokea ajali nyingi, na kuna watu walikufa pale kwenye daraja, inawezekana wengine wameanza kusahau, wanaozaliwa sasa hivi wanaweza kuona haya siyo chochote lakini hii ni ishara ya kupanda kwa uchumi wetu, uchumi unapopanda na miundominu inakuwa mizuri” amesema Rais Magufuli.

No comments: