Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole amefunguka kwa kumsifia Rais John Magufuli kwamba ni mwanaume pekee aliyeweza kuifanya Afrika nzima ikazizima kwa kuweza kupinga vitendo vya unyonyaji kwa taifa la Tanzania.
Polepole ameeleza hayo kupitia ukurasa wake maalumu wa facebook mchana wa leo huku akinukuu baadhi maneno aliyowahi kuyatoa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambayo yalikuwa wazi kabisa yakiongelea namna ya kujikomboa ili bara la Afrika kiujumla liweze kufikia uhuru wake wa kiuchumi.
"Leo Afrika nzima inazizima kwamba yuko mwanaume ambaye ameweza kusema imetosha 'enough is enough' siyo haki na ni unyonyaji kuchukua madini yetu katika namna ambayo haki yetu inapokwa. Ndugu Magufuli ana amini sana katika sekta binafsi na hasa katika ujenzi wa uchumi wa viwanda sambamba na sekta ya umma. Lakini ana amini zaidi katika sekta binafsi inayojiendesha kwa kanuni za maadili ikiwemo kulipa kodi. Anaamini katika uwekezaji kutoka nje, lakini unaotambua kwamba sisi ni taifa huru na tunayo haki ya kunufaika kutokana na utajiri wa rasilimali zetu", ameandika Polepole.
Aidha, Polepole amesema CCM imemleta Rais Magufuli katika wakati muafaka ambapo nchi ilikuwa inaelekea pabaya.
"Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemleta ndugu Magufuli wakati muafaka wakati tunamuhitaji zaidi mtu kama yeye. Ukisoma maelezo na nukuu za Mwalimu Nyerere katika maelezo yangu ya awali juu ya maono ya Mwalimu Nyerere utaungana nami kusema ile aina ya uongozi mpya katika bara la Afrika, Tanzania tumekuwa kinara wa kwanza na wengine watafuata ili bara la Afrika lirejeshe heshima yake ya uhalisia na asili", amesisitiza Polepole.
Kwa upande mwingine, Polepole amesema ipo siku ataeleza ni kwanini Rais Magufuli amekuwa zawadi katika taifa la Tanzania kwenye kipindi hiki.
No comments: