Kwa Rekodi Hii Yanga mtasubri sana


yanga_leo










Kesho Jumamosi Yanga inarejea Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kumenyana na Ndanda FC baada ya mechi mbili mfululizo walizocheza ugenini dhidi ya Njombe Mji na Majimaji ya Songea ambako wameambulia pointi nne.

Hata hivyo, kama unahisi Yanga wamefanya vibaya kwa kukusanya pointi hizo, inawezekana unajidanganya kwani kirekodi zinaweza kuwafanya waangue kicheko hapo baadaye.

Rekodi za misimu miwili iliyopita ya Ligi Kuu Bara zinaonyesha Yanga wamekuwa wakizitumia mechi zinazochezwa jijini Dar es Salaam kuwazidi kete Simba katika mbio za ubingwa.

Timu zote zina ugonjwa wa kuchemsha mechi za mikoani, lakini Yanga huwa haina mzaha inapocheza Dar jambo ambalo huifanya kumaliza ikiwa juu ya Simba ambayo imekuwa ikifanyia masihara mechi za jijini.

Katika msimu wa 2015/2016 ambao Yanga walitwaa ubingwa, ilipoteza pointi 17 tu kwenye ligi nzima baada ya kumaliza ikiwa na jumla ya pointi 73 wakati Simba ilimaliza ikiwa na pointi 62 huku ikipoteza pointi 28.
Katika pointi hizo 17 ilizipoteza Yanga, 11 ziliyeyukia nje ya Dar es Salaam ambapo ilifungwa na Coastal Union 2-0 huku ikitoka sare na timu za Majimaji, Mwadui, Mgambo na Prisons huku pointi sita tu zikipotea kwenye mechi zilizochezwa hapa jijini.

Katika msimu huo, kati ya pointi 28 ambazo Simba ilipoteza, saba ilipotezea ugenini huku 21 zikipotea katika mechi ambazo ilicheza Dar es Salaam ambapo ilifungwa mechi mbili na Yanga, ikafungwa na Toto Africans, Mwadui na JKT Ruvu huku ikitoka sare mechi mbili dhidi ya Azam.

Kwenye msimu uliopita, timu zote mbili zilipoteza pointi 22 ambapo Yanga ilipoteza 11 Dar es Salaam na kama hizo mikoani.

Simba yenyewe ilipoteza pointi 12 katika mechi ilizocheza jijini huku pointi 10 zikipotea kwa mechi za mikoani.

Katika hali ya kushangaza, Yanga haijawahi kupoteza mechi yoyote jijini ikiwa mwenyeji kwa miaka mitano na miezi sita (siku 2,022) tangu ilipopoteza dhidi ya Azam FC, Machi 10, 2012 ilipofungwa mabao 3-1.

No comments: