Kaimu Katibu mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Prof. Eleuther Mwageni ametoa tahadhari kwa wanafunzi wanaoomba kujiunga na vyuo vikuu kwa mwaka wa elimu 2017/2018 kuwa makini ili kuepuka kukosa nafasi.
Prof. Mwageni ameyasema hayo leo ikiwa imebaki siku moja kabla ya kufungwa kwa awamu ya pili ya kutuma maombi. Ameeleza namna ambavyo awamu ya kwanza imekuwa na changamoto ambapo takribani waombaji 180,640 walituma maombi.
“Mfumo wa sasa unahitaji muombaji kuwa makini sana kwasababu akicheza tu anapoteza nafasi, mfano ni awamu ya kwanza tulipokea majina 180,640 kutoka vyuoni lakini yalikuwa na makosa mengi watu walijirudia na kukosea majina yao tulipochambua tukapata majina 77,756 ambayo nayo bado yalikuwa na mapungufu ndio mana tulipitisha majina 44,627 na tukatoa muda kwa wengine watume maombi kwa usahihi katika awamu ya pili”, amesema Prof. Mwageni.
Katibu ameongeza kuwa waombaji wazingatie vigezo vya Vyuo na Kozi wanazoomba kulingana na ufaulu wao ili kuepusha kukosa nafasi kwenye vyuo wanavyoomba kutokana na alama zao kuwa chini wakati vyuo vina idadi ndogo ya wanafunzi huku wanafunzi waliofaulu vizuri wakiwa ni wengi.
Aidha Katibu amewataka waombaji waliochaguliwa kwenye vyuo zaidi ya kimoja kuthibitisha chuo kimoja ndani ya muda uliotolewa na endapo hawatafanya hivyo basi watapoteza sifa za kujiunga na elimu ya juu.
Amewaasa waombaji kutumia vizuri fursa hii ya awamu ya pili kwani hakutakuwa na muda zaidi wa kufanya udahili maana ratiba za masomo kwa mwaka wa elimu 2017/18 zinakaribia kuanza hivyo zoezi la udahili haliwezi kuendelea na endapo mwanafunzi mtarajiwa atakosea basi itabidi kusubiri hadi 2018/19
No comments: