TAKUKURU kufanya uchunguzi wa CCM mkoawa Mara

TAKUKURU kufanya uchunguzi uchaguzi wa CCM mkoawa Mara
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Mara inafanya uchunguzi kuhusu vitendo vya rushwa vinavyodaiwa kufanyika wakati wa uchaguzi wa Jumuiya ya umoja wa  vijana wa CCM (UVCCM)  katika wilaya ya Musoma mkoani Mara.

Katika uchaguzi huo ambao umefanyika Jumapili Septemba 24 Musoma, kumetokea vurugu baada ya makundi mawili hasimu kupigana katika kile kilichodaiwa kuwa kundi moja lilikuwa likitoa rushwa kwa wajumbe wake, ili waweze kumchagua kiongozi wao aliyekuwa anagombea nafasi hiyo.

Kamanda wa Takukuru wa Mkoa huo, Alex Kuhanda amesema wamepata taarifa za kuwapo kwa vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi huo na kwamba watatoa taarifa kamili baada ya uchunguzi kukamilika.

“Watakaobainika watakamatwa, kwa ajili ya kufikishwa mahakamani,” amesema Kuhanda

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo ambao waliomba hifadhi ya majina, wamesema hali hiyo ilitokea baada ya kundi la upande mmoja kugawa fedha kwa wajumbe ambao ndio wapiga kura katika uchaguzi huo.

Mashuhuda hao wamesema uchaguzi kwenye huo kulikuwa na vitendo vya rushwa ambavyo vilisababisha  baadhi ya wajumbe wa mkutano huo kuondoka bila kupiga kura kwa vigezo kwamba  uchaguzi huo ulikuwa siyo wa haki.



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara ACP Jafari Mohamed amesema mpaka sasa hajapokea taarifa zozote juu ya tukio hilo na wala hajapata taarifa yoyote ya watu waliojeruhiwa kutokana na vurugu hizo.

No comments: