Mwalimu atiwa mbaloni kwa kesi ya kumpa mwanafunzi mimba


Mwalimu wa shule ya msingi Samazi iliyoko Wilayani Kalambo mkoani Rukwa, anashikiliwa na polisi wa mkoa huo kwa tuhuma za kumbaka na kisha kumpa ujauzito mwanafunzi wa darasa la sita, mwenye umri wa miaka 15.

Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Judith Binyura amesema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi baada ya mwanafunzi huyo (jina limehifadhiwa) kumtaja kwamba ndiye aliyempa ujauzito huo.

"Tumekuwa na utaratibu kuwapima mimba watoto wa shule ili kubaini kama wana ujauzito,  sasa safari hii katika shule ya Samazi imegundulika kuwa mwanafunzi wa darasa la sita amepewa ujauzito na mwalimu wake," amesema .

Mratibu Elimu Kata ya Samazi, Daudi Sengo amesema mwalimu huyo alikuwa akimtuma mwanafunzi huyo kufanya kazi za nyumbani kwake kama kufua, kusafisha nyumba na kumpikia chakula cha jioni na kisha kufanya naye mapenzi mara kwa mara.

Ameongeza awali ilikuwa vigumu kuthibitisha kuhusu uhusiano wao wa kimapenzi hadi mwanafunzi huyo alipopimwa na kubainika ni mjamzito na alipobanwa na wazazi wake ndipo alisema amepewa na mwalimu huyo.

Binyura amefunguka kuwa kuna tabia ya baadhi ya walimu kufanya mapenzi na wanafunzi wao, jambo ambalo halikubaliki kwa kuwa linawaharibu watoto hao kisaikolojia na kuonya  kwamba hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wale wenye nia mbaya na watoto wa kike waliopo masomoni.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, George Kyando naye amekiri kwamba polisi inamshikilia mwalimu huyo na atafikishwa Mahakamani baada ya upelelezi kukamilika, ili sheria ichukue mkondo wake

No comments: