Dereva wa Dangote na Waethiopia 8 Wafikishwa Mahakamani

Watanzania  watatu akiwamo dereva wa kampuni ya saruji ya Dangote, Khalid Abdallah na wahamiaji wanane raia wa Ethiopia wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matano.

Miongoni mwa mashtaka  yanayowakabili ni kusafirisha kwa magendo binadamu na kuingia nchini kinyume cha sheria.

Mwendesha Mashtaka wa Uhamiaji, Novatus Mlay amewasomea mashtaka hayo leo Jumatano mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa.

Baada ya kusomewa mashtaka, raia hao wa kigeni wamekubali makosa yote yanayowakabili, huku Watanzania wakikana.

Raia hao wa Ethiopia, Solomon Ertiso, Gazahegn Tiroro , Haire  Latso, Thadius Lilanso, Dawit Habtam, Deznet Godebo, Feraru Gurana na Elioj Akola wanadaiwa Septemba 20 katika eneo la Kongowe wilayani Temeke walikamatwa wakiingia nchini bila ya kuwa na kibali.

Kwa upande wao, Khalid Abdallah ambaye ni dereva wa kampuni ya Dangote; Hussein Hamad Hassan na Jumanne Mtambo wanadaiwa Septemba 20 eneo la Kongowe wakiwa raia wa Tanzania walikutwa wakiwasafirisha wahamiaji hao haramu kimagendo.

Wanadaiwa waliwasafirisha wahamiaji hao kwa kutumia gari mali ya kampuni ya Dangote kwa kuwatoa Tanzania kwenda nchini Afrika Kusini.

Pia, wanadaiwa kuwaingiza ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania raia hao wa Ethiopia. Washtakiwa wamekana mashtaka.

Hakimu amewataka kuwa na wadhamini wawili kila mmoja ambao watasaini bondi ya Sh50 milioni kila mmoja. Kesi itatajwa Oktoba 10 na upelelezi imeelezwa haujakamilika. Walishindwa kutimiza masharti hayo hivyo wamepelekwa rumande.

Kwa upande wa raia wa Ethiopia, Mahakama imesema watasomewa maelezo ya awali Oktoba 10.

Wakati huohuo, raia 31 wa Ethiopia na wawili wa Tanzania wamepandishwa kizimbani mahakamani hapo wakikabiliwa na mashtaka matano ya kuingia nchini kinyume cha sheria.

Raia hao wa kigeni walikubali mashtaka na  watasomewa maelezo ya awali Oktoba 11.

Watanzania Ibrahim Abdallah ambaye ni dereva wa gari aina ya Nissan Civilian na kondakta Christopher Steven wanadaiwa Septemba 25 eneo la Toangoma wilayani Temeke walikutwa wakiwasafirisha  raia hao wa Ethiopia kimagendo kutoka Tanzania kwenda Afrika Kusini.

Washtakiwa walikana shtaka na upande wa mashtaka ulidai upelelezi haujakamilika. Kesi itatajwa Oktoba 11. Washtakiwa wamepelekwa rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

No comments: