Yanga Afiki Mbali kwa mwendo huu



UKISIKIA Yanga imefanya usajili wa kwanza kwenye dirisha dogo la mwezi ujao, basi nafasi hiyo ya kwanza ni straika namba 9 wa maana ambaye tayari mabosi wa klabu hiyo wameanza kutengeneza bajeti yake.
Kwa mastraika waliopo lolote linaweza kutokea kwao kama hawatajirekebisha kwenye mechi zilizobaki kabla ya dirisha hilo kufunguliwa Novemba 15.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Kamati ya Mashindano ya Yanga, zinasema kocha, George Lwandamina, amewaambia mabosi wake kwamba kabla hawajatia mguu katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, anahitaji straika aliye siriazi na mwenye uchu wa kutupia.
Mmoja wa wakubwa kwenye kamati hiyo, amedokeza kwamba Lwandamina amegundua mambo hayana uwiano katika kikosi chake ambapo kwenye mshambuliaji namba tisa yuko mmoja tu, Amissi Tambwe.
Takwimu katika kikosi cha Yanga zinaonyesha ina washambuliaji wanaocheza nyuma ya mshambuliaji wa kwanza, hao ni Donald Ngoma, Obrey Chirwa na Ibrahim Ajibu huku wale wa kati wakiwa wawili tu, Tambwe na Matheo Antony.
Hali hiyo imekuwa ikimweka Lwandamina katika wakati mgumu akilazimika kuwatumia Ngoma, Ajibu na Chirwa kwa wakati mmoja huku akilazimisha mmoja wao kucheza mshambuliaji kiongozi hali ambayo imekuwa ikiikosesha timu hiyo nafasi nyingi.
Lwandamina alipotafutwa jana Alhamisi alisema: “Tunayo shida ya washambulaiji wa mwisho katika kikosi chetu, nafikiri si kitu kipya kama unaona, ndiyo maana tulikuwa tunasubiri kurudi kwa Tambwe ambaye ameanza mazoezi sasa ingawa hatujajua atakuwa sawa baada ya muda gani.
“Hauwezi kuingia katika mashindano makubwa kama Ligi ya Mabingwa ukiwa na hali duni kama hii ya ufungaji, kwa hiyo kwanza kama makocha tunapambana kuhakikisha hawa tulionao tunawaongezea ubora.”
Mzambia huyo ambaye huwa ni nadra sana kwake kuzungumza na vyombo vya habari, aliongeza: “Katika hili yule tutakayeona bado hatujaridhika naye, tutaangalia cha kufanya huko mbele.”
Katika mechi tano za kwanza za Ligi Kuu Bara msimu huu zilizochezwa hadi sasa, Yanga imemudu kufunga mabao manne tu ikishinda mara mbili, kiwango kinachoashiria ubutu.
Unamkumbuka Kayembe?
Huyu ni yule beki Mkongomani aliyeletwa na Kabamba Tshishimbi ameandaliwa dakika 90 dhidi ya KMC Jumapili kwenye Uwanja wa Chamazi, Mbagala ili kumcheki kwa mara ya mwisho. Fiston Kayembe ambaye anaishi na Kabamba, Tumebaini kwamba kocha amekubali mambo yake na atampa mkataba.

No comments: