Misingi Ya Kuzingatia Katika Utunzaji Wa Vifaranga



Ufugaji wa kuku imekuwa ni kazi muhimu na inayokubalika katika jamii nyingi. Ni kazi isiyohitaji gharama kubwa sana, ambayo imekuwa na mafanikio kwa kiasi kikubwa kwa wanaiofanya kibiashara.
Tatizo ambalo limekuwa sugu na kusababisha hasara kwa wafugaji walio wengi, ni kutofahamu namna bora ya kuwatunza vifaranga kuanzia siku ya kwanza wanapoanguliwa hadi kuwa kuku wakubwa. Hali hii imekuwa ikiwasababishia wafugaji hasara na kuwakatisha tamaa.
Hii inatokana na wafugaji kuzingatia kuwa na banda na chakula tu, bila kuzingatia aina nyingine ya matunzo muhimu yanayohitajika kwa ajili ya kuwafanya vifaranga waishi na kukua wakiwa na afya.
Leo katika makala haya ya kilimo na ufugaji tunakuletea baadhi ya mambo muhimu ya kuzingatia kuanzia siku ya kwanza ili vifaranga wako wasipate madhara na hatimaye kufa;-
Mara baada ya kuanguliwa, vifaranga wawekwe sehemu yenye joto kwa wastani unaohitajika.
Hakikisha sehemu ya banda ulipowaweka vifaranga ni kavu, na isiyokuwa na vimelea.
Hakikisha vifaranga wote wanapata chanjo ya mahepe (mareks) siku ya kwanza.
Siku ya saba, vifaranga wachanjwe dhidi ya ugonjwa wa kideri.
Inapofika siku ya 14, vifaranga wachanjwe dhidi ya ugonjwa wa gumboro.
Rudia chanjo ya kideri katika siku ya ishirini na moja.
Siku ya ishirini na nane, rudia tena chanjo ya gumboro
Baada ya wiki nane, hakikisha kuwa vifaranga wako wanapata chanjo ya ndui.
Kwa kuzingatia mtiririko huo, utakuwa na uhakika kuwa kuku wako ni salama. Watakuwa bila tatizo, jambo ambalo litakupa uhakika wa kuwa na mazao bora, na hatimaye kupata faida.
Pamoja na hayo, hakikisha kuwa unazingatia lishe bora. Hii itasaidia kuwapa kuku afya njema na kuzalisha kwa kiwango kinachotakiwa. Misingi Ya Kuzingatia Katika Utunzaji Wa Vifaranga

No comments: