Hii ndo adhabu ya Simba ilio tolewa na TFF

Kikao cha kamati ya Masaa 72 ya shirikisho la Soka nchini TFF kimefikia maamuzi katika Masuala mbalimbali yanayohusu Ligi daraja la kwanza pamoja na Ligi kuu Tanzania Bara huku timu nyingi zikikumbana na adhabu mbalimbali ikiwemo Kupigwa faini pamoja na Wachezaji wao kufungiwa.
Kamati ya Bodi ya Ligi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imemuondoa Mwamuzi Msaidizi Grace Wamara kuchezesha Ligi Kuu ya Vodacom kwa kukosa umakini na kutomsaidia Mwamuzi, hivyo kusababisha akubali bao lenye utata la Stand United dhidi ya Mbeya City.
Wamara alikuwa Mwamuzi Msaidizi Namba Mbili kwenye mechi hiyo namba 31 iliyofanyika Septemba 24 mwaka huu kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga na wenyeji Stand United kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Klabu ya Stand United imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na wachezaji wake kuvaa jezi zenye namba tofauti na zile zilizosajiliwa. Wachezaji hao walivaa namba tofauti kwenye mechi namba 40 dhidi ya Simba iliyofanyika Oktoba 1 mwaka huu Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Simba imepigwa faini ya sh 500,000 (laki tano) kutokana na timu yake kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi katika mechi dhidi ya Mbao FC iliyofanyika Septemba 21 mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Kitendo hicho cha Simba ni ukiukaji wa Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu, na adhabu dhidi yao ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu. Pia Kamishna wa mechi hiyo, Maliki Tibabimale amepewa Onyo Kali kwa kutoripoti kitendo hicho cha Simba.
Singida United imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na mashabiki wa timu hiyo kuingia uwanjani kushangilia ushindi baada ya mechi dhidi ya Kagera Sugar iliyofanyika Septemba 23 mwaka huu Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Nayo Stand United imepigwa faini ya jumla ya sh. 1,000,000 (milioni moja) kutokana na washabiki wake kufanya vurugu kwenye mechi dhidi ya Mbeya City na Simba, zote zilichezwa kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

No comments: