Awali, ilielezwa kuwa Ngoma na Kamusoko, wangesafiri na timu kuelekea Bukoka kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar, lakini wasingecheza ili kuendelea kujiuguza kwa ajili mechi inayofuata dhidi ya Stand United.
Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja wa Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo ya SportPesa, Hafidh Saleh, alisema kuwa kikosi hicho kitaondoka kwa usafiri wa ndege na baada ya kufika huko wataendelea na mazoezi ili kukamilisha programu ya mechi hiyo ambayo wanahitaji kushinda na kurejesha morali kwenye kikosi chao.
Saleh alisema kuwa wamelazimika kuwaacha nyota wao Ngoma na Kamusoko ili waendelee na matibabu na mapumziko ambayo wamepewa ya wiki moja wakiwa hapa jijini.
"Timu haijaondoka leo (jana) kama tulivyotarajia, sasa tutasafiri kesho (leo), watakaobaki ni Ngoma na Kamusoko, lakini tunatarajia kuungana nao tukifika Shinyanga," alisema meneja huyo ambaye amedumu katika timu hiyo akichukua mikoba iliyoachwa na Emmanuel Mpangala.
Taarifa za ndani kutoka katika benchi la ufundi la Yanga, zinaeleza kuwa uamuzi wa kumuacha Ngoma unalenga kumuandaa mshambuliaji huyo na mchezo dhidi ya watani zao Simba utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa.
"Amekuwa majeruhi mfululizo, tumechukua uamuzi wa kumpumzisha kwa siku saba kuanzia Jumatatu kutokana na kuonekana majeraha yake hayajapona vizuri, ni muhimu akiwapo katika mechi dhidi ya Simba hapo Oktoba 28," alisema kiongozi mwingine wa Yanga.
Baada ya mechi dhidi ya Kagera Sugar inayofundishwa na Meck Maxime, mabingwa hao watetezi watasafiri kuelekea Shinyanga kuwafuata Stand United katika mechi nyingine ya ligi hiyo itakayofanyika Oktoba 22 kwenye Uwanja wa Kambarage.
No comments: