Habari mbaya kwa mashabiki wa Arsenal

Beki wa Arsenal Shkodran Mustafi aliumia kipindi cha kwanza katika mechi ambayo mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia Ujerumani walikamilisha rekodi ya asilimia 100 katika Kundi C la kufuzu kwa michuano ya mwaka ujao nchini Urusi kwa kuwalaza Azerbaijan 5-1.
Mustafi alichechemea na kuondoka uwanjani kutokana na kile kilichoonekana kama jeraha la misuli ya paja.
Aliumia muda mfupi kabla ya Ramil Seydaev kufungia Azerbaijan bao la kusawazisha.
Alisaidiwa kuondoka uwanjani na nafasi yake ikajazwa na Matthias Ginter.
Vijana hao wa Joachim Low walizinduka baada ya mapumziko ambapo kiungo wa kati wa Liverpool Emre Can alikuwa miongoni mwa wachezaji waliotikisa wavu.
Ujerumani wameshinda mechi zao zote 10 hatua ya makundi, na kufunga mabao 43.
Ndio timu ya kwanza Ulaya kushinda mechi zote 10 kati ya 10 michuano ya kufuzu baada ya Uhispania ambao mwishowe walishinda 2010.
Kiungo wa kati wa Schalke Leon Goretzka alifunga mabao mawili katika mechi hiyo iliyochezewa Kaiserslautern.
Winga Sandro Wagner anayechezea Hoffenheim naye aliibuka mchezaji wa kwanza kufunga mechi tano mfululizo katika mechi zake za kwanza tano kuchezea taifa tangu Ronald Worm mwaka 1978 alipofunga kwa kichwa.
Beki wa Chelsea Antonio Rudiger alijipatia bao la kichwa naye Can akafunga la mwisho kwa kombora kali hatua 25 kutoka kwenye goli.

No comments: