DR Congo: Waasi washambulia kambi ya UN

Wapiganaji wanaodaiwa kutoka Uganda wameshambulia kambi ya Umoja wa Mataifa kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kuua mlinda amani mmoja.
Shambulio hilo lilitokea katika kijiji kimoja karibu na mji wa Beni.
Msemaji wa walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo Florence Marchal amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema:
"Ninaweza kuthibitisha kwamba kumetokea shambulio katika kambi ya Monusco eneo la Mamundioma asubuhi hii na mlinda amani mmoja amefariki na wengine 12 kujeruhiwa."
Msemaji mmoja wa jeshi amelilaumu kundi la waasi la Allied Democratic Forces (ADF) kutoka Uganda, Reuters wanaripoti.
Wapiganaji wa ADF wamekuwa wakiendesha harakati zao karibu na mpaka kati ya DR Congo na Uganda.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, wanajeshi wa DR Congo walikabiliana na waasi hao kutoka Uganda eneo hilo siku ya Jumapili.
Siku moja awali, wapiganaji wa ADF walishambulia wahudumu 10 wa uchukuzi wa abiria wanaotumia pikipiki.

No comments: