Aina Ya Wateja Ambao Unatakiwa Kuwaepuka Mapema Kwenye Biashara Yako



Katika biashara ni kawaida kukutana na wateja wa aina tofauti tofauti na wateja wote kama tujuavyo ni muhimu na hutakiwi kumpa huduma yako mteja vibaya hadi ajisikie kwamba hataweza tena kuja kwenye biashara yako.
Mteja anatakiwa kujaliwa na kupewa huduma ambayo itamfanya ajione kwamba yeye ni mfalme kwa mazingira yoyote yale uliyo. Naamini hilo linawezekana sana kwako na unatakiwa kulifanya hilo katika uhai wote wa biashara yako.
Pamoja na kwamba mteja anatakiwa kujaliwa hivyo na ni muhimu, lakini, wapo aina ya wateja ambao inatakiwa kuwa nao makini sana katika biashara yako ili wateja hawa wasije wakaleta matatizo mengine kwenye biashara yako.
Wateja hawa ni wateja gani? Twende pamoja kujifunza;-
1. Wateja wanaolalamika sana.
Wapo wateja ambao kazi yao ni kulalamika sana. Wateja hawa wanalalamikia kitu hiki au kile kwenye biashara na kushindwa kuongea ukweli na kutatua changamoto za pamoja. Wateja hawa ni hatari sana kwenye biashara yako.
Wateja hawa ni moja ya wateja unaotakiwa kuwaepuka sana. Ni rahisi kukuharibia biashara yako na kusababisha wateja wengine wakukimbie kwa sababu ya kulalamika sana kusiko na msingi. Wateja wapya watafikiri kweli bidhaa zako ni mbovu kumbe la.
2. Wateja wanaokupotezea muda sana.
Pia wapo wateja ambao naweza kusema wao ni kama wana nia ya kukupotezea muda wako. Wateja hao si ajabu ukakuta wanauliza kitu fulani kwa muda mrefu sana na wanakiangalia na kukichunguza hata bila ya kununua pengine.
Unachotakiwa kuwa makini nacho hapa ni kuwa makini na wateja wa namna hii unapokutana nao ana kwa ana na hata wale unaokutana nao kwenye mitandao. Fanya hivi bila wao kujua kwamba unawaepuka.
3. Wateja wanaojiona wao ni maalumu sana.
Kuna wateja ambao wanapenda kujiona wao ni muhimu sana kuliko wateja wengine. Wateja hao ni rahisi tu kudai namba ya meneja wako au bosi wako ili wamweleze kile wanachokitaka wao wenyewe.
Kwa kifupi unapokuwa na wateja hawa nao ni wasumbufu sana na wanapenda kufanya kila wanachokitaka kwenye biashara yako ilimradi tu waonekane. Hivyo unatakiwa kuwa makini nao na kujua pia jinsi ya kuwakabili ii wasilete matatizo mengine.
4. Wateja wanaotaka kupatanisha kila kitu.
Sina shaka unawajua wateja ambao ukiwatajia bei ya kitu, wao ni kutaka kupatanisha na kuomba punguzo kila wakati. Unapokuwa na wateja wa namna hii wengi basi biashara yako itakuwa na usumbufu sana.
Vipo vitu ambavyo havihitaji kupatanishwa, bei na kila kitu kinaeleweka, sasa unapokuwa na mteja anayetaka kila kitu kiwekwe kwenye mapatano hapa unatakiwa pia uwe makini sana, vinginevyo utafanya biashara kwenye mazingira magumu.
Hawa ndio wateja ambao unatakuiwa kuwaepuka au kuwa nao makini sana kwenye biashara yako. Sijasema wateja hawa uwafukuze au uwajibu vibaya, ila unatakiwa kuwa nao makini ili wasije wakakuvurugia wateja wengine ambao ulitakiwa kuwa nao kwenye biashara.

No comments: