Watu wenye ulemavu kutoka Tanzania wanaoombaomba fedha katika mji wa Kerugoya nchini Kenya wamefikishwa kwenye Mahakama ya Kerugoya iliyopo katika Kaunti ya Kirinyaga huku msako mkali ukiendelea wa wengine.
Kati ya watu hao, watano walitozwa faini ya Sh20,000 au kwenda jela miezi mitatu kutokana na kosa hilo.
Hata hivyo wote hawakupata fedha hizo na watatumikia kifungo hicho huku mikakati ya kuomba warejeshwe kwao ikiandaliwa baada ya kumaliza kifungo.
Aidha, mmoja wao hakujibu mashtaka kwa kuwa ilitambulika kuwa ni bubu na ilimbidi hakimu amwelekeze mkuu wa mashtaka amtafutie mkalimani kesi yake itakaposikizwa Oktoba 3.
Walemavu hao watano wakiwa wanawake na mwanamume mmoja walishtakiwa kwa kuwa nchini Kenya kinyume cha sheria na kurandaranda ovyo kiasi cha kugeuka ‘ kero kwa raia’.
Wote watano walikiri kuwa waliingia nchini humo kutoka Tanzania na hawakuwa na nyaraka zozote za uraia wa Kenya.
Kwa mujibu wa mshirikishi wa masuala ya kiusalama katika eneo la Kati, Anne Ng’etich tayari walemavu wengine 150 wengi wao wana ulemavu unaosababishwa na ukosefu wa chanjo muhimu utotoni wamenaswa. Alisema baada ya uchunguzi kukamilika baadhi yao watafikishwa mahakamani huku wengine wakirudishwa kwao.
“Tumewakamata katika msako unaoendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali na tunatarajia kuwafikisha mahakamani wakati wowote kuanzia sasa. Pia tunapenda kuwaonya raia wengine wanaojihusisha na vitendo vya namna hii waachane mara moja Serikali iko macho,” alisema.
Akizungumzia kuhusu msako huo, mkurugenzi wa masuala ya watoto katika eneo la Kirinyaga Danson Omari alionya kuwa walemavu hao ‘wanawaajiri’ watoto wa maeneo hayo kuzurura na wao kuombaomba fedha kutoka kwa raia na kisha kuwalipa jioni jambo ambalo alisema ni kinyume na sheria za haki za watoto.
“Uchunguzi wangu kwa sasa unaonyesha kuwa walemavu hawa wanapenyezwa hapa nchini kutoka nchi jirani kupitia pwani,” alisema na kuongeza;
“Huwa wanapanda mabasi ya kutoka pwani yanayopitia miji ya Nyeri, Mwea na Kerugoya ili kuanza maisha mapya kama ya walemavu wenye haja ya kusaidiwa. Tutahakikisha tunawadhibiti.”
No comments: