Jana (jumatano Septemba 27) Wabunge nchini Uganda wamepigana ndani ya ukumbi wa Bunge wakiwa katika siku ya pili ya kikao cha kujadili muswada wa kuondoa ukomo wa miaka ya kugombea nafasi ya urais kwa mujibu wa katiba ya taifa hilo.
Kwenye kikao hicho kilichoongozwa na Spika wa Bunge, Rebecca Kadaga kulishuhudiwa ugomvi mzito wa wabunge kurushiana viti, kupigana makonde na kuharibu vipaza sauti.
Kwa bara letu la Afrika sio kitu cha kushangaza kusikia hivyo kwani imeshawahi kutokea Somalia, Kenya na Afrika Kusini ambapo Wabunge walishawahi kupigana tena wakiwa Live kwenye Runinga.
Tukio hilo kwa Tanzania linaweza kuwa geni kwenye macho yetu ukiachilia mbali matukio ya kawaida yanayotokea mara kwa mara kwenye bunge letu tukufu kama wabunge kutolewa nje kwa makosa ya kinidhamu na kadhalika.
Tufikiri kidogo kwa nini Wabunge wanafikia hatua ya kupigana Bungeni ile hali wana uwezo na muda wa kujadili kwa hoja na mambo yakaenda sawa?
Bila shaka yoyote ni hali ya kushindwa kuhimili hisia zao za uvyama na kusahau kuwa kuna wapiga kura wao ambao waliwachagua katika kuleta maendeleo katika jimbo husika.
Hii kasumba ya wabunge kutunishiana misuli au kupigana wakiwa kwenye vikao vya Bunge nchini Uganda tungependa wabunge wetu wa Bunge Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wachukulie kitendo hicho kama funzo kwao na kufikiria zaidi kushindana kwa hoja kuliko kutumia mabavu.
Kama haitoshi Wabunge ni wawakilishi wa wananchi hebu jiulizeni wananchi wa Wabunge waliopigana jana nchini Uganda wanachukuliwaje na Wananchi wao majimboni kwao ambao walikaa juani siku nzima kuwapigia kura? bila shaka ni picha mbaya, kama lengo ni kujenga taifa basi suluhisho sio kufikia hatua ya kupigana tena kwenye muhimili huo muhimu wa taifa.
Hivyo naelewa fika kuwa kwa haya yanayotokea kwa nchi jirani yabaki kuwa funzo kwa Wanasiasa wetu na nawashauri waheshimiwa Wabunge wabaki kwenye mstari wa kushindana kwa hoja na sio kuweka maslahi ya Vyama mbele kwani kwenye matukio yote ambayo wabunge wamekuwa wakipigana kwenye nchi za wenzetu hutokana na sababu za misimamo ya kivyama na sio kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
No comments: