Baada ya kuikomalia Yanga, kocha wa Mtibwa Sugar, Zuber Katwila amesema hataki kugawana pointi na Simba huku akiapa timu yake 'kufia' uwanjani Jumapili watakapokutana kwenye muendelezo wa Ligi Kuu.
Mtibwa itakuwa ugenini kwenye Uwanja wa Uhuru kuikabiri Simba ambapo timu zote zitashuka uwanjani zikiwa na pointi 11, lakini Simba inaongoza kwenye msimamo kwa idadi ya mabao huku Mtibwa ikiwa nafasi ya pili.
"Tunaiheshimu Simba, tunajua ni timu kongwe yenye uwezo siyo tu kifedha pia idadi kubwa ya mashabiki, ila kwenye mechi yetu ya Jumapili watatusamehe kwani hatuwezi kutoka Morogoro kwenda Dar es Salaam kisha turudi bila pointi," alisema kocha huyo.
Katwila alisema timu hiyo imepiga kambi Manungu, Turiani kujiweka sawa kwa mchezo huo itawasilia Dar es Salaam, Jumamosi mapema tu.
"Hatukuona sababu ya kwenda Dar es Salaam mapema kwa ajili ya kuiwahi Simba, tumeamua kubaki Manungu ambako tunaamini ndiko kuna 'dawa' ya ushindi Jumapili.
"Narudia tena, tunaiheshimu Simba, lakini hatuwezi kusafiri kwenda Dar es Salaam kisha turudi mikono mitupu, tunahitaji ushindi kwa namna yoyote ile na bila shaka vijana wangu watamshangaza 'mnyama'," alitamba kocha huyo.
Mtibwa itashuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kuing'ang'ania Yanga katika mchezo uliopita kwenye uwanja huo baada ya kutoka suluhu ya bila kufungana.
"Inshu ya Yanga imepita japo tulitaka pointi zote tatu lakini wenzetu wakakomaa tukagawana moja moja, lakini mechi ijayo tunachoangalia ni kuchukua pointi zote kwa Simba kwani inawezekana tukijipanga na vijana wangu uwezo huo wanao," alijinadi kocha huyo.
Katwila amekuwa na rekodi nzuri katika mechi tano alizoingoza Mtibwa tangu kuanza kwa msimu huu amesisitiza kwamba mikakati yake ni kuweka rekodi ya kutofungwa hadi msimu unamalizika huku akijinasibu kurejesha enzi za miaka ya 1999 na 2000 ambapo Mtibwa Sugar ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
No comments: