Kaya zaidi ya 30 wilayani Muleba mkoani Kagera hazina makazi baada ya nyumba zao kuezuliwa na upepo ulioambatana na mvua ya mawe.
Mvua iliyonyesha jana Jumanne jioni imesababisha maafa katika Kata za Buganguzi, Kamachumu na Mubunda.
Licha ya nyumba kuezuliwa, mashamba ya migomba yameharibiwa.
Diwani wa Buganguzi, Fortunatus Mwebesa amesema tathmini ya uharibifu inaendelea kufanyika kwa kushirikiana na wataalamu kutoka ngazi ya wilaya.
Amesema nyumba 22 zimeezuliwa pamoja na darasa katika Shule ya Sekondari Bukidea, huku nguzo tatu za umeme zikiangushwa na upepo.
Ofisa Kilimo wa Kata ya Mubunda, Christopher Nicholaus amesema uharibifu mkubwa umetokea kwenye mashamba ya migomba. Pia, nyumba mbili zimeezuliwa.
Amesema tathimini kujua kiwango cha hasara iliyosababishwa na upepo inaendelea na kwamba, Kijiji cha Kyaibumba ndicho kimeathiriwa zaidi.
Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Richard Ruyango amesema tayari ametembelea kata za Buganguzi, Ibuga na Mubunda.
Amesema taarifa kamili kuhusu maafa hayo itatolewa baada ya timu anayoiongoza kumaliza kazi ya tathimini.
Ruyango amesema hakuna taarifa ambayo imetolewa ya madhara kwa binadamu
No comments: