Umoja wa wanawake wajasiriamali (MOWE), wameandaa tamasha la 11 kwa wajasiriamali litakalofanyika kuanzia tarehe 24-30 Oktoba mwaka huu katika viwanja wa Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, lengo ikiwa ni kupanua wigo wa masoko pamoja na kuonyesha bidhaa na fursa mbalimbali za kijasiriamali zinazopatikana hapa nchini
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa kamati ya tamasha hilo, Bi. Zubeda Kiluwa amesema kuwa, tamasha hilo litakuwa na kauli mbiu isemayo‘Mwanamke mjasiriamali funguka shiriki kujenga Tanzania ya viwanda’
“Tunawaalika wanawake wote popote walipo kushiriki maadhimisho na maonyesho haya kwani yatawahusiha wadau mbalimbali wa maendeleo ya wanawake, Wizara pamoja na taasisi za serikali na mashirika binafsi,”alisema Kiluwa.
Tamasha hilo litafunguliwa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwaijage ambapo wadau watakaoshiriki kutoa elimu za kijasiriamali katika tamasha hilo ni pamoja na Wakala wa Usajili Biashara na utoaji leseni (BRELA), TRA, GSM, SIDO, TBS, TFDA pamoja na wawakilishi kutoka katika benki mbalimbali ambao kupitia semina hiyo watatoa elimu juu ya ujasiriamali.
Aidha Bi.kiluwa ameleza kuwa gharama zitakazotozwa kwa wajasiriamali watakaoshiriki katika maadhimisho hayo ni shillingi 50,000 kila mmoja, na kwa yeyote atakayeshiriki kwaajili ya uzinduzi, ununuzi na kujionea bidhaa mbalimbali hawatatozwa gharama yoyote.
Kwa upande wake mjumbe wa kamati ya tamasha hilo Bi.Anna Matinde amaesema kuwa tamasha hilo halitawahusisha wajasiriamali peke yake bali litawahusisha watu wote lengo likiwa ni kubadilishana mawazo ya kimaendeleo katika kuunga mkono sera ya Tanzania ya viwanda.
No comments: