Mkemia Mkuu atoa sababu za upimaji wa mkojo


SIKU chache baada ya kuzuka kwa mijadala yenye kuhoji sababu za kupimwa mkojo kwa watuhumiwa wa matukio mbalimbali, wakiwamo wa uchochezi, Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel Manyele, ametoa ufafanuzi na kueleza sababu kadhaa za kitaalamu za kufanyika kwa kazi hiyo.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, Prof. Manyele alisema msingi wa kufanyika kwa kazi hiyo, unaanzia kwa Jeshi la Polisi ambalo ndilo lenye jukumu la kupeleka sampuli za mkojo kwenye ofisi zake ili kupatiwa majibu kulingana na kile wanachotaka kifanyiwe uchunguzi dhidi ya watu wanaohusishwa na matukio mbalimbali.
 
Prof. Manyele alisema Jeshi la Polisi hupeleka sampuli za mkojo wa mtu ambaye wanadhani hawezi kufanya tukio alilofanya kwa akili zake bali kwa sababu nyinginezo, ikiwamo matumizi ya vitu vyenye kemikali zinazoweza kuathiri matendo ya mtu.

“Mtu kafanya kitu lakini mpelelezi anaona huyu hawezi kufanya kosa hili isipokuwa akili zake haziko sawa ndiyo maana wanakuja kwetu kupata uhakika,” alisema Prof. Manyele na kuongeza:

“Kuna matukio mtu anafanya kwenye jamii (ambayo) kwa akili za kawaida hadhaniwi kushiriki kufanya hivyo. Ndiyo maana wanatilia shaka kutaka kujua nini kilisababisha kufanya hivyo. Pengine ni dawa za kulevya, mirungi au bangi na ili kupata majibu ndiyo wanaleta sampuli tuzichunguze.”

Prof. Manyele alisema ofisi yake haiwezi kuchukua sampuli za watu kuwapima isipokuwa baada ya kupata taarifa kutoka Jeshi la Polisi au kwa watu binafsi, ambao nao huwa na sababu za msingi kufanya hivyo.

“Mimi siwezi kuwapima mkojo bali naletewa sampuli za kupima. Uamuzi ni wa Jeshi la Polisi… sisi tunatekeleza uamuzi huo ili upelelezi wao uende vizuri,” alisema.

Aidha, alisema makosa madogo huwa hayasababishi mtu kupimwa mkojo isipokuwa yale yanayotiliwa shaka kwa aliyetenda tukio husika.

Alitaja baadhi ya makosa yanayosababisha mtu kupimwa mkojo kuwa ni pamoja na ubakaji, ajali na pia makosa ya jinai kama matumizi ya silaha.

Aidha, Prof. Manyele alisema kuna matukio ya ajali yanayotokea ambayo ni tata kulingana na hali ilivyokuwa, ambayo huchangia kuchukua sampuli ya mkojo wa dereva na kumpima ili kubaini kama kilichotokea ni matokeo ya matumizi ya kemikali zenye kuathiri matendo ya mtu.

Prof. Manyele alisema pia waajiri wamekuwa wakipeleka wafanyakazi wao kupimwa sampuli ili kufahamu kama wapo sawa kwa ajili ya kuaminiwa kwa kazi wanazofanya.

“Wako waajiri wengi ambao wanapima mkojo wafanyakazi wao ili kujua kama wako sawa na wakati mwingine wanaleta maombi kwetu na sisi tunatuma watumishi wetu kwenda kuwachukua sampuli katika ofisi zao badala ya wao kuja kwetu,” alisema.

WAZAZI WAJITOKEZA
Prof. Manyele alisema pia katika upimaji wa sampuli za mkojo, wanaojitokeza kwa wingi ni pamoja na wazazi ambao huwapeleka watoto wao baada ya kuwatilia shaka juu ya matendo yao.

“Kwa sababu wazazi nao wapo bize na shughuli za ujenzi wa taifa, mara nyingi watoto wanaachwa wenyewe na haifahamiki wanafanya nini. Hivyo ni vyema wazazi wanapoona dalili wasizozielewa kwa watoto wao waje kwa Mkemia ili kupima sampuli,” alisema.

Hivi karibuni, mijadala ilishika kasi kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na sababu za kupimwa mkojo kwa baadhi ya wanasiasa waliokuwa wakituhumiwa kwa makosa mbalimbali, yakiwamo ya uchochezi. Kiini cha mijadala hiyo kilikuwa uhusiano kati ya upimaji mkojo na tuhuma za makosa ya uchochezi

No comments: