Unaanza mdundo mkali kisha sign tone ya producer Luffa, ni katika ngoma ya G Nako inayokwenda kwa jina la Arosto na ndani yake katika chorus ikisikika sauti ya Chin Bees.
Ngoma hiyo ambayo ilitoka May, 2016 ndio ikawa imekoleza moto katika uwezo wa Chin Bees na mashabiki wakazidi kumfahamu zaidi. Je baada ya hapo nini kilifuata?, twende pole pole.
Mnaowaita role model ni hatari, hatari take care, mnaowaiga wote mtapotea/
Ni line alizopitanazo Chin Bees katika chorus ya ngoma ya Nikki wa Pili ‘Role Model’ ambayo wamefanya refix ya ngoma ya Fat Joe ‘All The Way Up’. Ukaribu wake na Weusi na kazi walizofanya pamoja zimefanya jina lake kutokuwa ngeni masikioni mwa wale wanaosikiliza Bongo Flava.
Chin Bees ni nani?
Kwanza mwenyewe anakiri jina lake kuchanganya baadhi ya watu kutokana na ku-sound kama la Chidi Benz.
Katika mahojiano na Bongo5 alisema kitu hicho kilishawahi kutoka kwa producer Mesen Selekta ambaye katika computer yake alikuwa akitafuta wimbo wa Chidi Benz ft Ben Pol katika kutafuta akajikuta akipata ngoma ya Chin Bees ft Ben Pol na bila kujua alipocheza ndipo akagundua hakuangalia vizuri majina, tuachane na hilo.
Chin Bees ni msanii wa Bongo Flava ambaye kwa sasa yupo chini ya usimamizi wa Wanene Entertainment ambao alianza kufanya nao baada ya kuondoka studio kwa Nahreel ‘The Industry’ ambapo mwanzoni alikuwa akifanya kazi (kishikaji).
Chini ya Wanene Entertainment ameshatoa ngoma tatu official ambazo ni Pepeta, Nyonga Nyonga na Kababaye ambayo kwa sasa inafanya vizuri mtaani na kwenye media.
Chin Bees anajielezia kama msanii anayependa muziki mzuri na kufanya muziki mzuri pia, ukisikiliza ngoma zake zinajimbanua vizuri kama namna yeye binafsi anapokuwa akijielezea. Kiufupi ana tasnia yake pekee katika ulimwengu wake wa muziki.
Kitu hicho kimemfanya kujiamini na kusema hakuna msanii mwenye uwezo wa kufanya muziki aina trap kama yeye hapa Bongo, Chin Bees aliiambia XXL ya Clouds Fm kuwa anafanya kwa sababu anaona hamna msanii anaweza kufanya ipasavyo.
“Nafanya kutokana naona Bongo hakuna msanii anayeweza kufanya trap vizuri, wanafanya tu kwa sababu ya beat lakini kuna technique zake inabidi uzifuate. Off course wapo watu wanafanya trap lakini naona kama mimi nafanya better sana” alisesema Chin Bees.
“Kitu kingine amekuwa akieleza kuwa nyimbo zake karibia zote amekuwa haandiki zaidi ya kuangia studio na kuanza kuflow ila inatengemea yupo katika hali gani.
Katika mahojiano na Bongo5 alieleza kuwa karibia albamu nzima ambayo imeshakamilika alitumia mtindo huo, chakushngaza zaidi alieleza katika albamu hiyo hajafanya kolabo na msanii hata mmoja kwani anataka watu wawezi kujua uwezo wake. Kwa hayo machache bila shaka umepata picha Chin Bees ni msanii wa namna gani.
Sifa za ziada
Chin Bees kuna kitu cha pekee ambacho anacho katika muziki, kitu hicho ni uwezo wa kutengeneza melody ambayo ni rahisi watu kuikariri kitu ambacho hupelekea ngoma husika kuwa hit.
Moja ya ngoma ambazo zinatajwa kutoa ushirikiano huo ni ngoma ya Navy Kenzo ‘Kamatia Chini’ ambayo ilisumbua vilivyo mwaka jana na kupelekea kundi hilo kupata dili kutoka kampuni ya Airtel.
Kutambua mchango wake katika ngoma hiyo Navy Kenzo waliamua kumpa credit Chin Bees katika cover ya albamu yao ‘AIM’ iliyotoka mwaka huu. Hata hivyo Chin Bees aliona ni kitu ambacho kimechelewa, katika mahojiano na The Playlist ya Times Fm alisema kitu hicho kingetakiwa kufanyika wakati ngoma hiyo inatoka.
Pia mchango wake unahusika katika ngoma ya Vanessa Mdee inayokwenda kwa jina la Never Ever na ngoma ya Rosa Ree ‘Up In The Air’. Kumbuka nyimbo hizi tatu ambazo nimezitaja zilifanyika na Nahreel katika studio za The Industry ambapo mwanzoni Chin Bees alikuwepo. Tuachana na hilo.
Wasanii wengine: Msanii Madee kutoka Tip Top Connection, Madee katika mahojiano na Clouds Fm Top 20 alisema Chin Bees ni miongoni mwa wasanii wachache wa Bongo ambao kwa sasa wanajua kulitendea haki jukwaa vilivyo.
Alisema sifa ya ziada aliyonayo Chin Bees ni namna anavyotumia nguvu nyingi jukwaanii kitu ambacho mashabiki wake wamekuwa wakipenda.
Chin Bees na Weusi
Hapo awali nilieleza kuhusu kolabo ya G Nako na Chin Bees ‘Arosto’, pamoja na ile na Nikki wa Pili ‘Role Model’, hizi ni ngoma ambazo zimemfanya kuendelea kupiga hatu mbele katika muziki wake.
Nafasi hii ambayo member hawa wa kundi la Weusi wamempa Chin Bees mwenyewe amekuwa akitoa saluti na kila ukimuuliza kuhusu Weusi huwa anakujibu; wale ni mabroo.
Kama nilivyotangulia kueleza mara nyingi katika ngoma za Weusi G Nako amekuwa akisimama katika chorus, hata kama si ngoma ya kundi lakini mara kadhaa atasikika katika chorus ya Nikki wa Pili, Joh Makini au Bonta.
hivyo Chin Bees ameonekana kuwa na chemistry nzuri na ngoma za Weusi hasa katika upande wa chorus. Ndani ya miezi 16ameweza kufanya kolabo nne na Weusi.
Ukiachilia mbali ngoma mbili nilizozitaja hapo awali, kuna Sweet Mangi na Kihasara zote za Nikki wa Pili, utakumbuka mwaka 2015 Chin Chees alimshirikisha G Nako katika ngoma yake inayokwenda kwa jina Pakaza. Hivyo basi Chin Bees ana kolabo tano ndani ya Weusi, hii ni heshima kwake na muziki wake.
Kutokana na ukaribu na Weusi, hiyo juzi kipindi cha Planet Bongo kinachoruka EA Radio kilimuuliza Nikki wa Pili kuhusu kumsaini Chin Bees, hata hivyo kutokana na kundi hilo kutokuwa tayari kufanya hivyo, Nikki alijibu kuwa ukaribu wao na msanii huyo na kazi walizofanya zilipelekea kupata nafasi ya usimamizi chini ya Wanene Entertainment.
Vyovyote itakavyokuwa Chin Bees awepo ndani ya Weusi au lah!, bado heshima yake itakuwepo ndani ya kundi hilo na mbele ya mashibiki wa muziki wa Bongo Flava.
No comments: