Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro amewataka askari wa jeshi hilo kuchukua hatua ya kukomesha biashara ya Magendo inayofanyika mipakani, na kuonya kwamba wafanyabiashara wanaondekeza vitendo hivyo wanaikosesha serikali mapato ambayo yangetokana na kodi.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro anasema haya jijini Mbeya wakati akifanya mazungumzo na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, na baadaye akakagua gwaride na kuzungumza na Maafisa wa Jeshi la Polisi na Askari, huku akiwataka wananchi kutambua kuwa wanawajibu wa kulipa kodi, na kwamba tayari ametoa maelekezo kwa Jeshi la polisi kuwakamata wote wanaokepa kodi na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Aidha IGP Simmon Sirro amezungumzia suala la ujenzi wa vituo vya polisi, ambapo ameshauri Halmashauri kwa kutumia mapato yake ya ndani kwa kushirikiana na wananchi, kujenga vituo vya polisi kama wanavyojitolea kujenga vituo vya afya na vyumba vya madarasa.
Hata hivyo Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini amekemea tabia za mauaji zinazofanywa na baadhi ya wananchi katika mikoa ya nyanda za juu kusini kutokana na Imani za kishirikina na kwamba watakaokamatwa kufanya vitendo hivyo watachukuliwa hatua za kisheria huku akiomba viongozi wa dini na wanasiasa kusaidia kukemea vitendo hivyo.
No comments: