Iceland imekuwa nchi ndogo zaidi kuwahi kufuzu kwa Kombe la Dunia baada ya kuwalaza Kosovo 2-0 na kumaliza kileleni kundi lao la kufuzu kwa michuano hiyo itakayofanyika Urusi 2018.
Iceland, ambao walifika robofainali Euro 2016, baada ya kuwaondoa England hatua ya 16 bora, ni taifa la raia 335,000 pekee.
Ndiyo nchi ya kwanza kufuzu kwa Kombe la Dunia ikiwa na idadi ya watu ambao ni chini ya milioni moja.
Gylfi Sigurdsson wa Everton na Johann Gudmundsson wa Burnley ndio waliofungia taifa hilo Jumatatu.
Sigurdsson aliwapa matumaini kwa kufunga muda mfupi kabla ya mapumziko na kisa akamsaidia Gudmundsson kufunga bao la kuwahakikishia ushindi.
Iceland sasa wameshinda mechi saba kati ya 10 Kundi I la kufuzu kwa Kombe la Dunia.
Image captionMataifa madogo zaidi kuwahi kufuzu kwa Kombe la Dunia
Mkufunzi alihofia sherehe zingewaathiri
Mkufunzi wa Iceland Heimir Hallgrimsson alikuwa na wasiwasi kwamba angetatizika kuwapa motisha wachezaji wake baada ya kufana sana Euro 2016 nchini Ufaransa.
"Bia ya kwanza baada ya sherehe huwa si nzuri. Jambo ngumu zaidi lilikuwa kuendeleza ufanisi baada ya sherehe yetu kubwa kutokana na ufanisi Ufaransa," alisema.
"Na isitoshe, tulikuwa kwenye kundi lenye ushindani mkali lililokuwa na Croatia, Uturuki, Ukraine na Finland, nchi ambazo zinatuzidi kwa viwango vya soka.
"Ufanisi huu si mwisho bali ni safari ndefu ya kuelekea hadi kwenye mwisho wa safari."
Meneja wa Kosovo Albert Bunjaki amesifu sana Iceland kwa ufanisi wao na kusema kuwa hilo litatia moyo mataifa madogo.
"Naipongeza timu yote ya Iceland," amesema Bunjaki, ambaye taifa lake la Kosovo lina watu mara sita zaidi ya Iceland.
"Ni mfano mwema kwa mataifa madogo kama nchi yetu ambao hulenga kuwa na timu nzuri, yenye mpangilio mzuri, siku za usoni."
No comments: