Dhehebu la Shia Ithnasheria nchini leo limefanya matembezi ya amani yaliyoanzia kituo cha mabasi Ilala Boma na kuelekea mpaka msikiti Al Ghadiir uliopo Kigogo jijini Dar es salaam, lengo likiwa ni kuenzi na kukumbuka mchango wa Imam Hussein.
Akiyazungumzia matembezi hayo kiongozi mkuu wa Shia Ithnasheria Sheikh Hemed Jalala amesema kuwa ni matembezi yenye faida kwa waislamu na wasiokuwa waislamu kwa kumuenzi mjukuu wa pili wa Mtukufu Mtume Mohamad ambaye alifariki kwa kuwatetea wanadamu bila kuangalia itikadi zao za kidini, kikabila rangi, madhehebu nk.
Aliendelea kwa kusema kuwa ni kitendo cha ajabu sana kwa mtu kujitolea maisha yake kwa ajiri ya watu wengine, na kwa Imam Hussein alikufa akiwa yeye na familia yake na wengine ni watoto wadogo walio chini ya umri wa miezi sita wote waliuwawa na hii ni katika kukomboa dunia ya leo ambayo imebujikwa na mambo mengi yasiyo mazuri kama ugaidi, wizi, magomvi yasiyo na tija kwao.
Aidha Sheikh Jalala alisisitiza kuwa kitendo kilichofanywa na Imam Hussein
kinatufundisha wanadamu wa leo kujenge tabia ya kupendana, kuhurumiana, kusaidiana pamoja na kuheshimiana bila kuangalia itikadi zetu za kidini, kisiasa, kikabila nk. Kwani Imam Hussein alifanya ukombozi huo ili tusibaguane ila tuwe na umoja kati yetu sisi na majirani zetu hata na marafiki zetu na watu wote tunaoishi katika jamii moja.
Hivyo kupitia matembezi haya watanzania watajifunza mengi kwani hii sio kwa waislam tu bali watu wadini zote walipewa nafasi ya kujifunza mengi toka kwa Imam huyo ambaye aliishi katika kipindi kibaya ambapo hakukuwa na upendo, amani ilitoweka lakini yeye alisimama na kupingana na hali hiyo na siyo kwa faida yake tu bali ni kwa dunia nzima iweze kuwa huru na watu waishi vizuri kama mapenzi ya mungu yanavyotuamauru tufanye.
Na mwisho alipenda kuwasisitiza Watanzania kuendelea kulinda Amani tuliyo nayo, Umoja wetu pamoja na mshikamano na tusikubali kuvipoteza hivi vitu kwani ni nuru yetu tuliyopewa na mungu, kwani watanzania ni watu tusiojua kubaguana kikabila, kidini, kimaumbile hata kwa vipato vyetu bali tunaunganishwa na nguzo zetu kuu ambazo ni Amani, Umoja na mshikamano wetu.
No comments: