Miili ya Wanajeshi wa JWTZ Waliouawa DRC Yaagwa



Miili ya askari wawili wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliouawa nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) imeagwa tayari kwa kurejeshwa nchini.
Askari hao walikuwa kwenye operesheni ya ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa (UN). Habari zilizopatikana zilisema miili ya askari hao iliagwa jana.
JWTZ katika taarifa kwa umma juzi iliwataja askari hao kuwa ni Koplo Maselino Paschal Fubusi na Praiveti Venance Moses Chimboni. Taarifa ilisema askari wengine 12 walijeruhiwa katika shambulio lililofanywa na kundi la wapiganaji la ADF.
Taarifa ya Kurugenzi ya Habari na Uhusiano ya JWTZ ilisema askari hao walishambuliwa kwa kupigwa risasi na kundi la waasi Oktoba 9, wakiwa umbali wa kilomita 24 mashariki mwa mji wa Beni.
JWTZ ilisema UN inaandaa utaratibu wa kuirejesha miili ya askari hao na utakapokamilisha wataujulisha umma mapokezi, kuaga na mazishi yatakavyokuwa.
Wakati huohuo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amelaani mauaji hayo yaliyofanywa na wapiganaji wa ADF wenye asili ya Uganda.
Katika mashambulizi hayo, walinda amani wengine 18 ambao wako kwenye ujumbe wa UN unaojulikana kama Monusco walijeruhiwa. Katika taarifa ya Guterres kupitia msemaji wake, Stephane Dujarric ametuma rambirambi kwa Serikali ya Tanzania na familia za wafiwa. Pia, amewatakia heri majeruhi wapone haraka.
Katibu mkuu huyo ameitaka Serikali ya DRC kuanza mara moja hatua za uchunguzi kuhusu mauaji hayo. Kuhusu vikundi vya wanamgambo, Guterres amevitaka kusitisha mapigano na kutafuta suluhu kwa njia ya amani.
Amesema mashambulizi yoyote dhidi ya walinda amani yanaweza kuwa ni uhalifu wa kivita kama inavyoainishwa katika sheria za kimataifa.
Hii ni mara ya pili kwa Tanzania kupoteza askari waliopo kwenye operesheni ya amani nchini DRC.
Katika tukio la awali, askari mmoja aliuawa mwezi uliopita baada ya kushambuliwa na waasi.

No comments: