Kichuya sio mwenzetu ona maajabu alio fanya




WAKATI akina Haruna Niyonzima na Emmanuel Okwi wanatajwa kusajiliwa Simba, idadi kubwa ya mashabiki walidhani jina la Shiza Kichuya litamezwa na nyota hao, lakini winga huyo ni kama amegoma kabisa kupotezwa.
Kichuya alijizolea sifa kubwa kwa mashabiki kutokana na uwezo wake mkubwa aliouonyesha msimu uliopita, hasa akiifunga Yanga mara mbili lakini wengi wakadhani msimu huu jina lake litafukiwa na akina Okwi na Niyonzima ila hali imekuwa tofauti.
Kwanza msimu uliopita taarifa zilipozagaa kwamba Okwi atakuja kila mmoja aliamini kwamba jezi namba 25, ambayo anatumia Kichuya itabidi aiachie kwa Mganda huyo, kwani ndiyo aliyokuwa akiitumia kipindi cha nyuma lakini zoezi hilo halijafanikiwa.
Zoezi hilo halijafanikiwa kwa sababu Okwi ni kweli ametua Simba lakini amechukua jezi namba saba na kumwacha Kichuya kuendelea kutumia namba 25, huo ukiwa ni mtihani wake wa kwanza kuufaulu.
Mtihani mwingine ambao Kichuya anaonekana kuufaulu vizuri ni kutokana na kuwa kikosi cha kwanza huku pia akionyesha uwezo mkubwa na jina lake kuzidi kuwa kubwa na la kuogopwa.
Kwa sasa katika kikosi hicho cha Simba ukitaja majina matatu ya wachezaji muhimu ukaliruka jina la Kichuya, wenye Simba yao hawatakuelewa kwani kazi anayoifanya ni kubwa sana.
Winga huyo ndiye anayeshika nafasi ya pili kwa idadi ya mabao mengi kwenye timu yake, kwani katika michezo mitano waliyocheza mpaka sasa ana mabao matatu nyuma ya Emmanuel Okwi mwenye mabao sita, hiyo ikimaanisha kwamba kasi yake si ya kitoto.
Mashabiki wa Yanga wanamkumbuka vizuri Kichuya, kwani msimu uliopita aliwafanya kitu mbaya akisawazisha bao dakika za lala salama akipiga kona iliyojaa moja kwa moja wavuni mchezo wa mzunguko wa kwanza na mchezo wa mzunguko wa pili akifunga bao zuri na kuipa timu yake ushindi wa mabao 2-1.

No comments: