Simba na Yanga zinatarajiwa kukutana Oktoba 28 katika Uwanja wa Uhuru katika mchezo wa kwanza kukutana msimu huu wa Ligi Kuu Bara huku kila upande ukitarajia kukumbana na upinzani mkali.
Haruna Niyonzima anakutana kwa mara ya kwanza na timu yake hiyo ya zamani kwenye ligi baada ya mechi ya Ngao ya Jamii waliyocheza Agosti 23 ambapo Simba ilishinda kwa mikwaju ya penalti.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Niyonzima amesema kuwa, mchezo huo mara nyingi unakuwa mgumu na wa kiushindani lakini kwa upande wao wanajipanga kuweza kushinda mechi hiyo.
“Mechi ya Simba na Yanga mara nyingi inakuwa mechi ngumu na ni kubwa, hivyo kikubwa ni kuangalia ni jinsi gani tunaweza kujituma ili kufanikiwa kufanya vyema.
“Mara nyingi timu hizi zikikutana zinakuwa na ushindani wa hali ya juu tofauti na unavyocheza na timu nyingine, hivyo kunahitajika umakini wa hali ya juu, kwa upande wangu nimejipanga ili kuweza kushinda mchezo huo.
“Kwa sasa mimi siwezi kukizungumzia kiwango cha Yanga kwa kuwa kwa sasa nipo Simba, lakini ninachokiangalia ni ushindi tu,” alisema Niyonzima.
No comments: