Dereva wa Lissu awapa tabu Polisi


Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro amesema wanapata shida juu ya habari za kwamba dereva wa Lissu yuko nchini Nairobi anatibiwa kisaikolojia wakati kwenye magazeti anaonekana akiwa ameng'aa.
IGP Sirro amezungumza maneno hayo leo alipokuwa ziarani mkoani Mtwara ambapo ametuma salamu za kumtaka dereva wa Lissu kurudi nchini kulisaidia jeshi hilo katika kukamilisha upelelezi wake juu ya tukio la shambulio kwa kiongozi huyo.
“Yule kijana kwenye picha ukimwona yuko vizuri tu, sasa wanaposema anapata huduma ya kisaikolojia wakati kwenye magazeti anaonekana hii inatupa changamoto. “Mtu anasema anatibiwa kisaikolojia lakini kila siku nikiona magazeti anaonekana anawaka, inanipa tabu.”amesema IGP Sirro.
IGP Sirro amesema miongoni mwa anaohitajika kuhojiwa ni dereva wa Lissu ambaye awali viongozi wakuu wa CHADEMA walitoa taarifa na kueleza kwamba dereva huyo yupo jijini Nairobi akipatiwa matibabu ya kisaikolojia kutokana na shambulio aliloshuhudia kwa macho yake kupigwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu.
Pamoja na hayo IGP Sirro amewataka waandishi wa habari kuwasilisha taarifa hiyo kwa umma akisema, “Kimsingi waandishi wa habari naomba mlipeleke hili sisi tuna uchungu sana na mheshimiwa Tundu Lissu, tunamheshimu ni mtu muhimu kwa Watanzania na sisi tunataka tuwapate waliofanya lile tukio lakini ushirikiano ni mzuri ili kufanikiwa,”
Nakuongeza kwamba "Ndugu zangu, mheshimiwa Lissu amepigwa risasi na watu tunaowatafuta, huyo kijana kuja kwake kutatusaidia kupata majibu ya mambo mengi,” ameongeza IGP Sirro.
Tundu Lissu ambaye yupo Jijini Nairobi nchini Kenya kwa ajili ya matibabu, alishambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi Septemba 7 nyumbani kwake Area D mjini Dodoma na watu wasiojulikana. 

No comments: