Kiungo wa Simba, Mnyarwanda, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima, amesema kuwa watahakikisha wanafanya kila liwezekanalo ili kuondoka na alama tatu kwenye mchezo wao ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Stand United.
Niyonzima ameyasema hayo baada ya kuishuhudia timu yake ikitoka sare ya kufungana mabao 2-2 na Mbao FC katika mchezo wa ligi hiyo uliopigwa Alhamisi iliyopita kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.
Akizungumzia mchezo wao ujao ambao watacheza Jumapili ijayo dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Niyonzima amesema sare yao dhidi ya Mbao ilikuwa imepangwa hivyo sasa wanajipanga kurejesha wembe wa ushindi siku hiyo.
“Hata kama ukimleta Zidane au nani, kama Mungu ameandika droo inakuwa droo, timu yetu ni nzuri na tuliweza kufunga mabao mawili lakini tulishindwa kuyalinda japo tulitengeneza nafasi nyingi. Watu wanatakiwa kukumbuka kuwa, tupo ugenini japo tunafahamu tulitakiwa kushinda lakini hata kuipata hii pointi moja si mbaya"
Niyonzima aliendelea kufafanua kuwa
“Tunajipanga kufanya vizuri mechi ijayo kuhakikisha tunaondoka na pointi tatu, kuzikosa pointi tatu mechi iliyopita wala hakijaharibika kitu, tutafanya vizuri tu mechi ijayo,” amesema Niyonzima.
Simba kwa misimu kadhaa wamekuwa hawana matokeo mazuri katika dimba hilo la Kirumba ama wakipata matokeo ya ushindi kwa taabu wanapokutana na timu za jiji hilo tangu wakati huo wa enzi za Pamba, Toto Africans na sasa Mbao FC.
No comments: