Kipa mkongwe wa Kagera Sugar, Juma Kaseja, amekiri kikosi chao hicho kimeanza vibaya msimu huu, lakini akatamka kuwa, wakishinda mechi moja tu basi ndiyo safari yao ya kuanza kufanya vizuri msimu huu itakuwa imeanza rasmi.
Kagera Sugar kwa sasa ndiyo inayoshika mkia kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi moja baada ya kucheza mechi nne na kutoka sare moja, huku ikipoteza tatu.
Kaseja ambaye kwa nyakati tofauti aliwahi kuzitumikia Simba na Yanga, amesema anaamini upepo huo mbaya utaondoka kikosini kwao pindi watakapopata ushindi wao wa kwanza katika ligi hiyo kwani kwa sasa benchi lao la ufundi linafanyia makosa yanayojitokeza kwenye mechi zao.
“Makosa tunayofanya katika mechi zetu benchi la ufundi linayaona, hivyo wanapata nafasi ya kuyafanyia kazi kwa lengo la kufanya vizuri katika ligi ya msimu huu. Bado ni mapema kusema msimu huu hatutafanya vizuri kwa sababu ndiyo kwanza tumecheza mechi nne tu, hivyo basi naamini tukipata ushindi mmoja tu katika mechi zetu zijazo, tutarudi kwenye mstari na kufanya vizuri msimu huu,” alisema Kaseja.
No comments: