Rais Magufuli amewazungumzia wabunge wawili wa (CHADEMA) Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema pamoja na Mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki Mhe. Joshua Nassari kuwa ni wabunge halali wa majimbo hayo kwa kuwa wananchi ndiyo waliwachagua.
Rais Magufuli amesema hayo leo aliposimamishwa na wananchi wa Sangisi katika kata ya Akeri nje kidogo ya Mji wa Arusha akiwa njiani kurejea jijini Dar es Salaam leo Asubuhi na kusema yeye atabaki kuwa Rais wala hawezi kubadilika na kuendelea kuwatumikia Watanzania wote.
"Uchaguzi umeshakwisha sasa ni maendeleo mliamua mkamchagua Magufuli na ndiyo Rais na mimi nitakuwa Rais wala sibadiliki na nitawatumikia Watanzania wote, mliamua mkamchagua Mhe. Lema wa CHADEMA kuwa Mbunge wenu yule ni Mbunge halali, mkaamua kumchagua Nassari kuwa Mbunge wenu ni Mbunge halali kwa hiyo tushikamane sisi kama Watanzania kuleta maendeleo yetu uchaguzi ulikwisha tusubiri mwaka 2020" alisema Rais Magufuli
Mbali na hilo Magufuli amewataka Watanzania kuleta maendeleo ya kweli bila kubagua vyama na kubagua dini zetu na bila kubagua makabila na kusema yeye kama kiongozi wa nchi hajaweza kuwabagua na ndiyo maana anafanya mambo ya maendeleo katika majimbo hayo ikiwa ni pamoja na kupeleka barabara
No comments: