Hofu yatanda mechi ya Manchester United

Wiki hii michuano ya Champions League inaendelea kupigwa, siku ya Jumatano kutakuwa na mchezo kati ya Manchester United ambao tayari hii leo wamesafiri kuelekea Urusi kuwakabili CSKA Moscow.

Mchezo huu umekuja kipindi ambacho mashabiki wa Urusi na wa Uingereza siku za karibuni wamekuwa katika hali ya mtafaruku kila mmoja akimuonesha mwenzie ubabe jambo linalozua hofu kuhusu mchezo huu.

Mwaka jana katika michuano ya Euro nchini Ufaransa mashabiki wa Urusi na wa Ufaransa walileteana fujo kubwa hali iliyojenga kisasi baina ya mashabiki wa mataifa haya mawili.

Tayari mashabiki 2000 wanaotoka nchini Uingereza kwenda kuangalia mchezo huo nchini Urusi  wameonywa kuhusu tishio la kutokea kwa fujo wakati wa mchezo huo na kushauriwa kuchukua tahadhali.

Manchester United nao wamewaonya mashabiki zao kuhusu kuvalia jezi za klabu hiyo mtaani na kuwasisitiza kufuata sheria za nchi hiyo watakapokuwa mjini Moscow.

Mwenyekiti wa masuala ya usalama wa chama cha soka cha Urusi amewaonya wageni kwamba wasitarajie kuonewa huruma kama wakikiuka sheria za ushangiliaji za nchini humo kwani yeyote atakayekosea atapewa adhabu kali bila kujali wapi anatokea.

“Sitaki kumtisha mtu lakini nataka kuwaonya wale watakaokuja hapa kwamba wasijaribu kufanya aina yoyote ya fujo na wakifanya hivyo tutawapa adhabu kali ikiwemo kubaki hapa” alisema Vladmir Markin.

No comments: