China imeyaambia makampuni ya Korea Kaskazini yaliyo nchini mwake kufunga, wakati inajaribu kutekeleza vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya taifa hilo.
Makampuni hayo yatafungwa ifikapo mwezi Januari. Pia makampuni yanayomilikiwa na nchi hizo mbili yatalazimika kufunga.
China ambayo ni mshirika pekee mkuu wa Korea Kaskazini tayari imepiga marufuku biashara ya nguo na kupunguza bidhaa za mafuta.
Hatua hiyo ni sehemu ya hatua za kimataifa kujibu jaribio la sita na lenye nguvu la nyuklia.
- Marekani yaitaka China kuikanya Korea Kaskazini
- China yaitaka Korea Kaskazini kusitisha majaribio ya makombora
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ambapo China ni mwanachama, lilipiga kura kwa wingi kuunga mkono vikwazo vipya tarehe 11 Septemba.
Wizara ya biashara nchini China ilisema kuwa imeweka siku ya mwisho ya siku 120 tangu kupitishwa kwa azimio hilo kwa kampuni yoyote ya Korea Kaskazini iliyo nchini China kufunga.
Korea Kaskazini imetengwa kisiasa na kiuchumi na sehemu kubwa ya biashara yake inafanya na China.
China tangu jadi imekuwa ikimtetea jirani wake huyo, lakini imemkashifu vikali kwa majaribio yake ya nyuklia na matamshi yake.
Mapema mwaka huu ilizuia kuingizwa kwa mkaa wa mawe kutoka Korea Kaskazini na bidha zingine.
Baada ya marufuku ya bidhaa za nguo, Korea Kaskazini imepoteza mapato yake kadha ya pesa za kigeni.
China imekuwa ikishinizwa kuchukua hatua kutoka kwa rais wa Marekani Donald Trump, ambaye ameipongeza na mara nyingine kupinga sera za China.
Trump pia amehusika kwenye vita vya maneno na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un, akimtaja kama "mtu wa makombora" aliye kwenye mikakati ya kujitia kitanzi.
Alisema kuwa hana lingine ila kuiharibu kabisa Korea Kaskazini ikiwa atalazimika kuilinda Marekani na washirika wake.
No comments: