Soma Kauli alizo tolewa AJIBU



WINGA wa zamani wa Yanga ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Soka la Vijana la Yanga, Said Maulid ‘SMG’ amesema kama Ibrahim Ajibu ataendelea kujituma basi atafika mbali na anaweza kuuzwa Ulaya.
SMG aliyewahi kucheza Simba pia, alisema Ajibu akiendelea kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu Bara, basi njia itakuwa nyepesi kwake kucheza Ulaya.
Ajibu alijiunga na Yanga katika msimu huu wa Ligi Kuu Bara akitokea Simba baada ya mkataba wake kumalizika kwa dau la shilingi milioni 50 huku akipewa gari aina ya Toyota Brevis.
Ajibu hivi sasa ni tegemeo kwenye kikosi cha Yanga kinachonolewa na Kocha George Lwandamina na tayari amefanikiwa kufunga mabao mawili kati ya mechi tano alizocheza ambayo yaliamua ushindi wa timu.
Akizungumza katika kipindi cha Spoti Hausi kinachorushwa na Global TV Online, SMG alisema anaheshimu kiwango cha Ajibu ndani ya uwanja kutokana na msaada anaoutoa tangu atue Yanga.
SMG alisema Ajibu anatakiwa kutosikiliza kelele za mashabiki wa timu yake ya zamani na badala yake kuelekeza nguvu katika kazi yake.
“Ajibu ni kati ya wachezaji wenye vipaji na naheshimu uwezo wake uwanjani, kiukweli ninapenda aina yake ya uchezaji katika kutengeneza na kufunga mabao.
“Ninaamini kama akiendelea kufanya hivi Yanga kwa msaada anaoutoa katika timu, basi ninamtabiria atafika mbali ikiwezekana kucheza soka la kulipwa Ulaya,” alisema SMG.
Stori: Wilbert Molandi,

No comments: