Ndege hizo za kuangusha mabomu zilipaa kutoka kisiwa cha Marekani cha Guam
Marekani kwa mara nyingine imefanya mazoezi ya kijeshi kwa pamoja na Korea Kusini, ambapo ndege zake mbili za kivita za kuangusha mabomu zimepaa juu ya rasi ya Korea.
Ndege hizo za kutekeleza mashambulizi aina ya B-1B zimepaa angani pamoja na ndege za kivita za Korea Kusini aina ya F-15K.
Ndege hizo zimetekelesha amzoezi ya kurusha makombora kutoka angani hadi ardhini katika maji ya bahari ya KOrea Kusini.
Mazoezi hayo yamefanyika huku wasiwasi na uhasama kati ya Marekani na Korea Kaskazini kuhusu mpango wake wa nyuklia ukizidi.
Pyongyang majuzi ilitekeleza jaribio lake la sita la silaha za nyuklia na pia imerusha makombora kupitia anga ya Japan mara mbili miezi ya karibuni.
Ndege hizo za Marekani zilipaa kutoka kisiwa chake cha Guam katika Bahari ya Pacific Jumanne usiku kabla ya kuingia anga ya Korea Kaskazini na kufanya mazoezi katika Bahari ya Mashariki na Bahari ya Manjano, jeshi la Korea Kusini limesema.
Mazoezi hayo yalikuwa sehemu ya mpango mkubwa "wa kuzuia kupitia vitisho" vitendo vya Korea Kaskazini, jeshi hilo lilisema.
Marekani imesema jeshi la wana anga la Japan pia limeshiriki mazoezi hayo.
Rais wa Marekani Donald Trump alikutana na maafisa wakuu wa usalama Jumanne usiku kujadili njia za kukabili vitisho vya Korea Kaskazini, ikulu ya White House ilisema.
Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un wamejibizana wiki za karibuni.
Trump Agosti alisema Kim Jong-un atajuta sana, na upesi sana, iwapo atatishia kisiwa cha Guam tena
Akihutubu Umoja wa Mataifa Septemba, Trump alisema Bw Kim yupo kwenye "safari ya kujiandamiza".
Kim naye alimweleza Trump kama mzee aliyepungukiwa na uwezo wake wa kiakili na kuahidi kumfunza adabu kwa moto.
Jumatano, mbunge wa Korea Kusini alisema wadukuzi kutoka Korea Kaskazini walidukua mitambo na kuiba shehena kubwa ya nyaraka za siri za jeshi la Korea Kusini, ikiwa ni pamoja na mpango wa kumuua Kim Jong-un.
Aidha, kulikuwa na mpango wa hatua za kukabili Korea Kaskazini wakati wa vita ambao ulikuwa umeandaliwa an Marekani na Korea Kusini kwenye nyaraka hizo.
Wizara ya Ulinzi ya Korea Kusini ilikataa kuzungumzia madai hayo ambayo yalikanushwa na Korea Kaskazini.
Mambo muhimu kuhusu hali ya kijeshi rasi ya Korea
No comments: