Mama aliyeua na kujeruhi wanaume wawili kwa kisu, mahakama yamuachia huru na kumpa jina la ‘SIMBA’



Mama mmoja nchini Afrika Kusini ameachiwa huru na mahakama baada ya kuua kijana mmoja na kuwajeruhi wawili waliokuwa wanambaka binti yake.
Mama huyo aliyebatizwa jina la ‘Simba wa Kike’ na jaji wa mahakama moja mjini Tarkastad, katika jimbo la Eastern Cape, kwa kitendo chake cha ujasiri cha kumuokoa mwanaye amesema, siku ya tukio saa mbili usiku alipigiwa simu na majirani akiambiwa atoke nje amuokoe binti yake amevunjiwa nyumba na watu wasiojulikana.
Mama huyo mwenye miaka 56 ambaye jina lake limehifadhiwa kwa sababu za kiusalama amesema alitoka haraka akiwa ameshika kisu na kukimbia nje ambapo alikuta tayari vijana hao wameshavunja chumba cha binti yake mwenye 27.
Akihojiwa na kituo cha runinga cha M-Net mama huyo amesema alipoingia alikutana na vijana watatu waliokuwa wenye nguvu wakiwa wanamshambulia mtoto wake.
Ndipo alipomuawahi na kumchoma kisu mgongoni kijana mmoja aliyekuwa juu ya binti yake na kufa hapo hapo na kuwajeruhi wawili kwenye maeneo ya mikono na tumboni.
Baada ya tukio hilo vijana wawili walikimbia wakimuacha mwenzao na mama ikamlazimu kutembea umbali wa kilomita 3 kwenda kutoa taarifa polisi.
Hata hivyo mama huyo alikamatwa na polisi na mtoto wake kupelekwa hospitali huku mwili wa mbakaji ukichukuliwa kwa ajili ya uchunguzi.
Mama huyo wakati anajitetea mbele ya mahakama amesema ni kweli alifanya tukio hilo kwa kukusudia kutokana na jeshi la polisi kushindwa kuwadhibiti vijana hao wahalifu.
Akiendelea kujitetea mbele ya jaji mama huyo amesema tabia ya vijana kubaka wananwake katika kijiji hicho imekuwa kama desturi kwani wahalifu wanatekeleza vitendo hivyo na hakuna hatua zinazochukuliwa za kisheria.
Akitoa ushuhuda amesema mwezi wa septemba mwaka huu tayari wanawake wanne wamebakwa na wahalifu wanajulikana lakini hakuna wa kuwachukulia hatua za kisheria.
Vijana wawili waliojeruhiwa na mama huyo tayari wameshikwa na polisi na binti huyo ameshapona na alikuwa moja ya mashahidi katika kesi hiyo.
Tukio hilo limetokea septemba 2 mwaka huu katika kijiji cha Idutywa, jimbo la Eastern Cape nchini Afrika Kusini.

No comments: