KOCHA wa Simba, Joseph Omog amesisitiza kwamba tangu anasaini mkataba alifahamu atakuwa chini ya presha kubwa Msimbazi kutokana na ukubwa wa klabu hiyo na wingi wa mashabiki.
Omog ameenda mbali zaidi na kusema kwamba, atapendelea kama akiona shabiki mmoja ambaye amejitokeza na kumpinga kwa hoja zenye mashiko kuwa timu haichezi vizuri au kuna kitu gani aambacho hakiendi sawa.
Amesisitiza kuwa kelele na presha zinazopigwa pembeni ni hali ya kawaida kwenye mashindano ndio maana amewaambia wachezaji wake watulize akili wafanye kazi na hilo ndio sababu wanaongoza ligi.
“Tangu nakubali kuifundisha Simba nilitambua kuwa nitakuja kukutana na kelele za mashabiki tena zaidi ya hizi ambazo wanasema wakati huu,” alisema kocha huyo wa zamani wa Azam.
Omog, ambaye amewahi kuinoa kwa mafanikio AC Leopards ya DR Congo alisema; “Nimekuja kufanya kazi na ndio maana tumeanza msimu vizuri na tunaongoza ligi hadi sasa, kwa upande wangu naona hao mashabiki wanapiga tu kelele wala hawana sababu ya msingi ambayo inawafanya waongee maneno ambayo si mazuri.
“Natoa ruhusa kama kuna shabiki wa Simba mwenye pointi za msingi ambazo zinamfanya kuongea maneno mengi juu ya maendeleao ya timu msimu huu ajitokeze, anikosoe kwa hoja,” alisema.
“Tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri msimu huu na kwa kikosi nilichokuwa nacho nina imani nitatimiza lengo letu kuu,” alisema Omog ambaye nahodha wake ni Method Mwanjali wa Zimbabwe.
No comments: