Wanawake 100 wa BBC: Vitu tisa ambavyo huenda hukujua vilivumbuliwa na wanawake

Unapoulizwa kuwataja wavumbuzi maarufu zaidi duniani, huenda usiwasahau Thomas Edison, Alexander Graham Bell na Leonardo da Vinci.
Lakini Mary Anderson je? Au Ann Tsukamoto?
Huenda usiwe unayajua majina yao lakini hao ni wavumbuzi wawili tu kati ya wavumbuzi wengi wanawake ambao walihusika katika kuvumbua vitu vingi muhimu kwa maisha ya kawaida na pia uvumbuzi muhimu wa kisayansi.
Msimu wa Wanawake 100 wa BBC mwaka huu tunaangazia makala za wanawake wenye ushawishi na wanaowahamasisha wengine.
Aidha, tutafanya jambo la kuwapa watu changamoto.
Wanawake kutoka pande mbalimbali duniani watatakiwa kuvumbua vitu ambavyo vinaweza kutatua baadhi ya shida nyingi wanazokumbana nazo.
Soma hadi chini kwa maelezo zaidi kuhusu Wanawake 100 wa BBC, na kwa uhamaisho zaidi, hapa chini ni vitu tisa muhimu vilivyovumbuliwa na wanawake.
1. Programu za Kompyuta - Grace Hopper
Baadaya kujiunga na jeshi la wanamaji la Marekani wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, Grace Hopper alipewa kazi ya kuunda kompyuta mpya, iliyopewa jina Mark 1.
Hakuchukua muda mrefu kabla yake kuwa miongoni mwa watengenezaji wa programu za kompyuta (maelezo ya kufanyiwa kazi na kompyuta) wakati wa miaka ya 1950.
Alishiriki katika kuunda compiler, programu ndogo ambayo iliweza kufasiri maelezo ya kompyuta ya kuandikwa na kuyafanya kuwa maandishi ambayo kompyuta ingeyasoma.
Hilo lilirahisisha utengenezaji wa programu za kompyuta na kubadilisha jinsi kompyuta zilikuwa zinafanya kazi.
Hopper alisaidia kuvumisha neno "de-bugging" ambalo bado hutumiwa katika kuandika programu za kompyuta hadi wa leo, baada ya nondo kuondolewa kutoka kwenye kompyuta yake.


Alifahamika zaidi kama "Amazing Grace", na aliendelea kufanya kazi na kompyuta hadi alipostaafu kutoka kwenye jeshi akiwa mwanajeshi wa jeshi la wanamanaji aliyehudumu akiwa na umri wa juu zaidi, akiwa na miaka 79.
Illustration of Dr Shirley Jackson and a mobile phone
2. Kumtambua mpiga simu (Caller ID) naKuichelewesha simu(Call waiting)- Dkt Shirley Ann Jackson
Dkt Shirley Ann Jackson ni mwanafizikia ya nadharia Mmarekani, ambaye utafiti wake miaka ya 1970 ulichangia kuanzishwa kwa huduma mbili, moja ya kumtambua anayepiga simu na nyingine ya kuichelewesha simu.
Ufanisi wake katika teknolojia ya mawasiliano uliwawezesha wengine kuunda kipepesi ambacho kingeweza kusafiri na mtu, nyaya za kusafirisha data kwa kutumia mwanga na mitambo ya sola.
Ndiye mwanamke wa kwanza Mwamerika wa asili ya Afrika aliyepata shahada ya uzamifu (udaktari) kutoka Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Massachusetts (MIT) na mwanamke wa kwanza Mwamerika wa asili ya Afrika kuongoza katika chuo kikuu kinachoongoza kwa utafiti.
Illustration of Mary Anderson and some windscreen wipers
3. Kipangusa kioo cha gari - Mary Anderson
Siku moja majira ya baridi mwaka 1903, Mary Anderson alikuwa ziarani New York alipogundua kwamba dereva wake gari lililokuwa limembeba alilazimika kila wakati kufungua kioo cha upande wake ili kupangusa theluji kwenye kioo cha mbele cha gari.
Kila wakati alipofungua kioo, hewa baridi iliingia ndani ya gari.
Anderson alianza kufikiria suluhu - bada lenye mpira ambalo lingesongeshwa mtu akiwa ndani ya gari, na mwaka 1903 alisajilisha uvumbuzi wake.
Lakini kampuni nyingi hazikupokea kifaa hicho upesi, nyingi zikiamini kwamba kingetatiza madereva.
Anderson hakufaidi kutokana na uvumbuzi wake, hata baada ya vipangusa vioo vya magari kuanza kutumiwa katika magari yote.
4. Betri za ktuumiwa anga za juu - Olga D Gonzalez-Sanabria
Betri zinazodumu na chaji muda mrefu za nickel-hydrogen zimesaidia sana kutoa nishati kwa Kituo cha Kimataifa cha Anga za Juu.
Kwa hivyo ni muhimu sana.
Olga D Gonzalez-Sanabria, ambaye asili yake ni Puerto Rico, alisaidia kuasisi teknolojia ambayo ilisaidia kuundwa kwa betri hizo miaka ya 1980.
Kwa sasa, yeye ni mkurugenzi wa uhandisi katika Kituo cha Utafiti cha Glenn katika Shirika la Anga za Juu la Marekani (Nasa).
line
100 Women Challenge logo
Wanawake 100 ni nini?
Katika Msimu wa Wanawake 100 wa BBC, huwa tunawataja wanawake 100 wenye ushawishi na wanaowahamasisha wengine kutoka kila pembe ya dunia kila mwaka. Mwaka 2017, tunatoa changamoto kwao kukabili matatizo manne makuu yanayokabili wanawake siku hizi - vikwazo katika kupanga ngazi katika jamii, kutojua kusoma na kuandika miongoni mwa wanawake, kudhalilishwa wakiwa maeneo ya umma na kunyanyaswa michezoni.
Kwa usaidizi wako, watatafuta suluhu kwa matatizo hayo na tunataka ushiriki kwa kutoa mawazo hayo. Tupate katika FacebookInstagram na Twitter na utumie kitambulisha mada #Wanawake100

5. Mashine ya kuosha vyombo - Josephine Cochrane
Mtumbuizaji Cochrane alitaka mashine ambayo ingeosha vyombo vyake haraka kuliko wafanyakazi wake wa nyumba, na bila kuvivunja.
Mashine yake ilijumuisha mota iliyokuwa inazungusha gurudumu ndani ya mtungi wa kuchemsha maji ulioundwa kwa madini ya shaba nyekundu.
Ilikuwa ndiyo mashine ya kwanza kabisa ya kuosha vyama iliyotumia presha ya maji.

Mume mlevu wa Cochrane alikuwa ameacha deni kubwa sana wakati wa kifo chake. Hilo lilimchochea kuhakikisha amesajili uvumbuzi wake mwaka 1886 na akafungua kiwanda chake mwenyewe cha kuunda mashine hizo.
Illustration of Marie Van Brittan Brown and CCTV cameras
6. Mfumo wa usalama nyumbani - Marie Van Brittan Brown
Marie Van Brittan Brown, mwuguzi ambaye mara nyingi alikuwa akikaa pekee nyumbani, alifikiria kuhusu kituo ambacho kingemfanya kujihisi salama zaidi nyumbani.
Akiwa pamoja na mumewe Albert, Van Brittan Brown aliunda mfumo wa kwanza wa kuhakikisha usalama nyumbani kutokana na ongezeko la visa vya uhalifu na desturi ya polisi kuchelewa kufika eneo la uhalifu miaka ya 1960.
Kifaa chake kilikuwa na vitu vingi, kilikuwa na kamera ambayo ilitiwa nishati na mota. Kamera hiyo ilipanda na kushuka na kutazama nje kupitia tundu la kuchungulia.
Kulikuwa na skrini kwenye chumba chake cha kulala ambacho kilikuwa pia na kitufe cha kufungulia king'ora.
Illustration of Ann Tsukamoto and a petri dish
7. Kutenganisha seli tete - Ann Tsukamoto
Uvumbuzi wake ulisajiliwa rasmi 1991 na tangu wakati huo, kazi yake Tsukamoto imesababisha kupigwa hatua kubwa sana katika kufahamu mfumo wa damu wa wagonjwa wa saratani, jambo ambalo mwishowe huenda likasaidia kugunduliwa kwa tiba.
Tsukamoto kwa sasa anaongoza utafiti kuhusu ukuaji wa seli tete na ni mmiliki mwenza wa vitu vingine saba vilivyovumbuliwa.

8. Kevlar - Stephanie Kwolek

Mwanakemia huyu alivumbua nyuzi zisizo na uzito sana ambazo hutumiwa katika fulana zinazozuia risasi kupenya pamoja na mavazi mengine ya kukinga mwili dhidi ya risasi.
Tangu uvumbuzi wake mwaka 1965, nyuzi hizo ambazo zina nguvu mara tano kuliko chuma, zimesaidia kuokoa maisha ya watu wengi. Hutumiwa na mamilioni ya watu kila siku.
Hupatikana kwenye glavu za nyumbani, simu za rununu, ndege na hata katika madaraja.

9. Monopoly - Elizabeth Magie

Mwanamume kwa jina Charles Darrow hutambuliwa kama mwasisi wa mchezo maarufu zaidi wa ubao duniani, lakini kanuni zake zilivumbuliwa na Elizabeth Magie.
Magie alitaka kuonyesha matatizo ya ubepari kwa mchezo mpya ambapo wachezaji wakebadilisha pesa na mali bandia.
Muundo wake ambao aliusajili mwaka 1904 uliitwaThe Landlord's Game.
Mchezo wa Monopoly tunaoujua kwa sasa ulichapishwa mwaka 1935 na Ndugu wa Parker, ambao waligundua kwamba Darrow hakuwa mwasisi wa mchezo huo na kwamba alikuwa ameununua kutoka kwa Magie kwa $500 (£385).
Kuna wanawake wengi sana wavumbuzi ambao bado hawajatambuliwa, kwa hivyo tusaidie kuwafahamu kwa kutuandikia kupitia FacebookInstagram na Twitter, kwa kutumia kitambulisha mada #100Women au #Wanawake100.

No comments: