Mshambuliaji hatari zaidi anapoona nyavu, Amissi Tambwe ameanza mazoezi na Kocha George Lwandamina ana nafasi ya kuongeza upana wa kikosi chake.
Tambwe ameanza mazoezi jana katika Uwanja wa Uhuru baada ya kuwa amefanya mazoezi ya pekee kujiandaa na kuungana na wenzake.
Pamoja na Tambwe, beki wa pembeni wa Yanga, Hassan Kessy ambaye alikuwa anasumbuliwa na majeraha baada ya kupata ajali ya bodaboda, naye ameanza mazoezi akionyesha yuko vizuri tofauti na awali.
Daktari wa Yanga, Edward Bavu amethibitisha wawili hao kuanza mazoezi ingawa jana walikuwa wakikimbia pembeni ili kuhakikisha wanakuwa vizuri zaidi na uhakika, watakaa nje Yanga ikiivaa Mtibwa Sugar, kesho.
"Tambwe mwenye majeraha ya goti na Kessy yeye majeraha ya ajali ya bodaboda wote wapo fiti na leo (jana) waliendelea kufanya mazoezi yao ya binafsi kwa ajili ya kujiweka fiti ambao wataukosa mchezo wa keshokutwa Jumamosi dhidi ya Mtibwa kwa kuhofia kujitonesha licha ya kuanza mazoezi," alisema Bavu.
No comments: