Serikali kuwapatia ulinzi Wabunge

SERIKALI imetangaza kuanza mchakato wa kuwapatia ulinzi wabunge nchini ikiwa ni wiki tatu tangu mwakilishi wa wananchi wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kunusurika kifo baada ya kupigwa risasi tano mwilini na miguuni na watu wasiojulikana.

Wabunge hawatambuliwi kisheria kupewa ulinzi kama ilivyo kwa viongozi kadhaa wa serikali.

Akizungumza kwenye mahojiano na redio moja ya jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwingulu
Nchemba, alisema masuala ya ulinzi kwa viongozi yapo kwa mujibu wa Sheria, lakini kuna baadhi ya watu ambao hawajatambulika kupewa ulinzi.

"Kwa sasa suala hilo la ulinzi kwa waheshimiwa wabunge linashughulikiwa na tutaongeza ulinzi kwenye maeneo yote ya viongozi na kufanya doria za mara kwa mara," alisema Mwigulu.

"Hata Lissu alipodai kutishiwa tuliongeza ulinzi, lakini shida ni jinsi alivyokuwa anatoa taarifa hadharani."

Watu waliomshambulia Lissu ambaye amelazwa katika Hospitali ya Nairobi, Kenya, kwa risasi mfululizo kutoka katika bunduki inayodhaniwa kuwa SMG, wanadaiwa kuwa katika gari nyeupe aina ya Nissan.

Lissu alishambuliwa na watu hao saa 7:30 mchana akiwa ndani ya gari lake, akiwa amefika nyumbani maeneo ya Area D, Manispaa ya Dodoma, baada ya kutoka kwenye kikao cha Bunge. Imedaiwa risasi tano zilimpata tumboni na miguuni.

Mashuhuda wa shambulizi hilo la kwanza la aina yake dhidi ya Mbunge nchini, walisema Lissu wakati akiingia kwenye lango la nyumba yake alikuwa ameongozana na magari mawili.

Shuhuda mmoja ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini kwa sababu za kiusalama, alisema aliona mtu mmoja akishuka kutoka moja ya magari mawili hayo na kwenda kwenye Toyota Landcruiser ya Lissu ambapo alimshambulia kwa risasi na kisha kupanda gari na kuondoka.

Alisema hali hiyo ilizua taharuki ya watu kukimbizana huku milio zaidi ya risasi ikisikika hewani kabla ya majambazi hao kutokomea kusikojulikana.

"Baada ya kupigwa niliona gari zilizokuwa zimefuatana naye zikitoka kwa kasi huku namba zake zikiwa zimefichwa," alisema shuhuda huyo.

Alieleza kwenye gari alikuwapo Lissu na dereva wake aitwae Simon ambaye alitoka na kuanza kuomba msaada, ili akimbizwe hospitalini, alisema shuhuda huyo.
Alieleza kuwa baada ya hali ya taharuki kutulia walijitokeza wasamaria wema ambao ni wanawake, waliosaidiana na dereva huyo kumwingiza kwenye gari dogo kwa ajili ya kumkimbiza Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma.

ONGEZA ULINZI
Waziri Mwigulu alisema: "Baada ya (Lissu) kusema anatishiwa maisha tuliongeza ulinzi, lakini shida ni jinsi alivyokuwa anatoa taarifa hadharani. Hii ingeweza hata kuwapa mwanya wale waliokuwa wanapanga njama za kumdhuru kujipanga zaidi.

"Lissu alipotaja gari iliyokuwa inamfuatilia niliagiza lisakwe na hilo lilifanyika na watu walikamatwa na kuhojiwa.

"Lakini ilibainika gari lilikuwa tofauti na lile alilolitaja na gari hilo lilionekana halijafanya safari yoyote kwenye maeneo ambayo Lissu alikuwapo."

Aidha, waziri huyo alisisitiza kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea, lakini kutokana na mazingira ya sasa hawatasema chochote hadi hapo uchunguzi utakapokamilika.

"Tunahakikisha kuweka nguvu kubwa kutafuta ukweli wake na undani wake kwa sababu tukio hili halikubaliki na ni tukio linaloudhi," alisema Mwigulu.

"Kuna vitu vingi ambavyo bado tunasita kuvisema hadharani, tunaomba wananchi wawe na imani na kazi ambayo tunaendelea kuifanya na watapewa taarifa."

Aidha, Waziri Mwigulu alisema Serikali inaendelea kupata taarifa za maendeleo ya afya ya Lissu kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya, ingawa yeye hajakwenda kumwona

No comments: