Rais Magufuli awalilia na kuwatumia rambi rambi watanzania waliopoteza maisha kwa ajali Uganda


Responsive image
Ajali iliyohusisha basi dogo aina ya Coaster na Lori aina ya fuso nchini Uganda na kuua Watanzania 13
Rais Dkt. John Magufuli amemtumia salamu za rambirambi aliyewahi kuwa Naibu Waziri na Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Mpwapwa mkoani Dodoma, - Gregory Teu kufuatia vifo vya watu 13 ambao ni ndugu wa familia yake waliopoteza maisha katika ajali ya gari iliyotokea nchini Uganda.
Watu hao wamefariki dunia baada ya basi dogo walilokuwa wakisafiria kutoka kwenye sherehe ya harusi kugongana na lori jana usiku katika barabara ya Masaka nchini Uganda wakiwa njiani kurejea Tanzania.
Katika salamu zake Rais Magufuli amesema kuwa amepokea taarifa ya vifo hivyo kwa mshtuko mkubwa na kutoa pole pia kwa wanafamilia, ndugu na jamaa wote walioguswa na msiba huo na kuwataka wanafamilia wote kuwa na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na wapendwa wao na watu muhimu waliowategemea.
Rais Magufuli pia amewaombea marehemu wote wapumzike mahali pema na pia amewaombea majeruhi wote wanaopata matibabu huko nchini Uganda wapone haraka na kurejea nyumbani.
Akizungumza kwa njia ya simu na TBC, Naibu Balozi wa Tanzania nchini Uganda, -Elibariki Maleko amesema kuwa Ubalozi huo kwa kushirikiana na serikali ya nchi hiyo unaendelea na taratibu ili kuhakikisha miili ya Watanzania hao 13 inasafirishwa kuja nchini haraka iwezekanavyo.

No comments: