Kasi ya Okwi yaiweka pabaya Yanga


Kasi ya mabao ya mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi, imeiweka Yanga katika wakati mgumu kwani hata wakishinda dhidi ya Ndanda FC leo Jumamosi, hawawezi kupanda na kuwa juu ya Simba ambayo imeapa kuondoka na taji msimu huu.

Yanga imefunga mabao matatu tu hadi sasa msimu huu na kama itahitaji kuishusha Simba kwenye nafasi ya pili leo itahitaji kushinda kwa mabao tisa ama zaidi, jambo ambalo hawajaonyesha dalili ya kulifanya tangu msimu huu uanze huku moja ya sababu inayotajwa na mashabiki mitaani ikiwa ni kukosekana kwa Simon Msuva aliyeuzwa Morocco.

Simba ambayo ilipata sare ya 2-2 na Mbao FC juzi Alhamisi, ina pointi nane zinazoweza kufikiwa na watani zao Yanga leo, lakini yenyewe ina wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa, jambo ambalo linawanyima Yanga nafasi ya kuwashusha.

Mchawi wa Simba msimu huu amekuwa Okwi ambaye amefunga nusu ya mabao yaliyofungwa na klabu hiyo. Simba imefunga mabao 12 mpaka sasa lakini sita amefunga Mganda huyo peke yake.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara wapo katika nafasi ya saba kwa pointi tano, lakini wakiishinda Ndanda watafikisha nane kama za Simba, ishu itabaki kwenye mabao.

Hata hivyo, Mtibwa Sugar bado ina nafasi kubwa ya kuendelea kusalia kileleni kama itapata sare ama ushindi ugenini dhidi ya Ruvu Shooting ambayo tangu kuanza msimu huu haijashinda hata mara moja.

Mtibwa ina pointi tisa kileleni na ikipata sare itafikisha 10 ambazo zinaweza kufikiwa na Azam pekee ambayo kesho Jumapili itacheza na Lipuli inayofundishwa na nyota wa zamani wa Simba, Selemani Matola.

Kama Mtibwa itapoteza kesho itazipa upenyo Mbeya City na Singida United kupanda juu endapo zitashinda michezo yao kwani zitafikisha alama tisa sawa na vinara hao, hata hivyo dakika 90 ndiyo zitazungumza ukweli.

Habari mbaya kwa Mtibwa ni kwamba msimu uliopita haikupata ushindi wowote mbele ya Ruvu kwani ilipoteza mchezo mmoja na ikatoa sare mwingine.

Kwa upande mwingine timu za Mtibwa, Yanga na Singida United ndizo zilizofunga bao kwenye kila mchezo msimu huu sambamba na Mbao, hivyo wikiendi hii zitakuwa na kazi kubwa ya kuendeleza moto wao huo.

Kocha wa Yanga, George Lwandamina, amewaambia viongozi wasimlipe chochote kwanza yeye bali wamalizane na wachezaji watengeneze matokeo uwanjani kwa kuanzia na mechi ya leo dhidi ya Ndanda. Na wakafanya hivyo.

Rekodi zinaonyesha Yanga haijawahi kuwa na mchezo mwepesi dhidi ya Ndanda kwani katika mechi sita walizokutana, mabingwa hao wameshinda mbili tu na wamepoteza mara moja.

Mechi dhidi ya timu hizo mbili pia zimekuwa na uhaba wa mabao kwani katika michezo hiyo sita ni mabao 11 tu yamefungwa ikiwa ni wastani wa pungufu ya mabao mawili kwenye kila mchezo.

Hata hivyo, rekodi zinaibeba Yanga pindi inapokuwa Dar es Salaam kwani katika michezo minne waliyokutana, wameshinda mara mbili na nyingine mbili kumalizika kwa sare.

Kwa mujibu wa mazoezi ya jana ya Yanga, nahodha Thaban Kamusoko atarejea uwanjani leo akicheza sambamba na Raphael Daudi na Papy Kabamba Tshishimbi huku safu ya ushambuliaji ikiendelea kuwa chini ya Donald Ngoma, Ibrahim Ajibu na Obrey Chirwa.

Mechi nyingine wikiendi hii, leo Jumamosi Mwadui atacheza na Prisons, Majimaji na Njombe Mji huku kesho Jumapili Singida ikicheza na Kagera Sugar wakati Stand United ikiwa wenyeji wa Mbeya City

No comments: