Tanzania ni nchi iliyo katika ukanda wa kitropiki, ambapo kiasi kikubwa cha sumu kuvu huzalishwa hasa katika mazao ya nafaka kama vile mahindi, karanga na kunde.
Sumu kuvu inayojulikana kitaalamu kama mycotoxins, ni aina za kemikali za sumu zinazozalishwa na aina ya ukungu au fangasi wanaoota kwenye mbegu za nafaka kama vile mahindi, mbegu za mafuta kama karanga, jamii ya kunde, mazao ya mizizi na pia vyakula na malisho ya wanyama.Aflatoxin 1
Sumu kuvu pia hupatikana katika bidhaa za mifugo kama vile maziwa, mayai na nyama pale ambapo chakula kinacholiwa na mifugo kitakuwa kimechafuliwa na sumu hizo.
Vilevile baadhi ya sumu kuvu hupatikana kwenye maziwa ya mama anayenyonyesha iwapo atakula chakula kilichochafuliwa na sumu hizo.
Ingawa kuna aina nyingi za fangasi ambao wanaweza kuota na kukua katika vyakula hivi, ni fangasi wachache tu ambao hutoa sumu kuvu.
Sumu kuvu haiwezi kuonekana kwa macho, haina harufu, haina kionjo na wala haina rangi. Ukungu unaotokana na sumu kuvu unaweza kuwa na rangi ya kijani, chungwa, kijivu, au njano chafu na unaweza kutoa harufu ya uvundo.
Ukungu huo unaotoa sumu kuvu, hustawi ikiwa mazao yamekumbwa na ukame yakiwa shambani au kushambuliwa na wadudu waharibifu na yakahifadhiwa kwenye ghala lenye joto na unyevu katika kiwango cha juu.
Vyakula vinavyoweza kupata sumu kuvu
AflatoxinVyakula ambavyo vinaweza kuambukizwa sumu kuvu ni kama vile mahindi na unga wake, karanga na mazao yanayotokana na karanga, muhogo, nyama, mayai na maziwa (vyakula vitokanavyo na mnyama au ndege aliyeambukizwa pamoja na mazao yao) na vyakula vya mifugo vyenye mbegu zilizoambukizwa au nyasi au vyakula vya mifugo vya kutengenezwa).
Hatari zitokanazo na sumu kuvu
Binadamu au mnyama anaweza kula sumu kuvu kupitia vyakula vinavyochafuliwa na ataathiriwa kutegemeana na kiasi cha sumu kuvu kilichomo.
• Tafiti nyingi za kisayansi vimeonesha uhusiano wa sumu kuvu na athari mbalimbali za kiafya kama vile saratani, hasa ya ini, kushusha kinga ya mwili, kudumaa hasa kwa watoto, sumu kwenye figo na vifo kwa binadamu na wanyama ikiwa viwango vya sumu kuvu ni vikubwa. Baadhi ya sumu kuvu hutoka kwa mama kwenda kwa mtoto akiwa bado tumboni.
• Athari za kiafya zinaweza kujitokeza baada ya muda mrefu wa matumizi. Sumu inaweza kujirundika na kuendelea kuwa nyingi mwilini kidogo kidogo kulingana na mtu atakavyokuwa anaendelea kula vyakula vilivyo na sumu hiyo.
• Mbali na madhara ya kiafya, uchafuzi wa sumu kuvu huathiri pia uhakika wa chakula na biashara. Bidhaa za kilimo zikipatikana na sumu kuvu iliyozidi kiwango kinachokubaliwa, hazikubaliwi kwenye masoko ya nje ya nchi na badala yake zinateketezwa.
Njia za kudhibiti maambukizi ya sumu kuvu
Kuna njia mbalimbali ambazo mkulima anaweza kuzitumia ili kupunguza uchafuzi wa sumu kuvu katika mazao yake yakiwa shambani au baadaAflatoxin 2 ya kuvuna. Njia hizo ni kama zifuatazo;
• Lima aina za mazao yenye ukinzani dhidi ya kuvu wanaotoa sumu kuvu (kama inapatikana).
• Vuna mazao yakiwa yamekauka vizuri kama inavyoshauriwa na afisa wa kilimo na pia epuka kutia majeraha katika mazao yako.
• Usianike mazao yako kwenye udongo mtupu. Tumia turubai au aina nyingine ya vifaa vya kuanikia au kukaushia mazao
• Wakati na baada ya kuvuna chambua na kuondoa mbegu zilizooza, zilizovunjika, zilizotobolewa au kuharibiwa na wadudu pamoja na zile zilizobadilika rangi.
• Hifadhi mazao mahali pakavu na pasipo na joto. Hakikisha mazao yaliyohifadhiwa hayanyeshewi na mvua au kulowa maji.
• Hifadhi mazao kwenye ghala linaloruhusu mzunguko wa hewa.
• Zuia wadudu waharibifu na kuvu kwa kunyunyiza madawa yaliyokubalika na kushauriwa na wataalamu wa kilimo.
• Unaweza pia ukakoboa mahindi na kuchambua vizuri kabla kuyahifadhi ili kuondoa yale yanayoelekea kuwa na uchafuzi wa sumu kuvu ambayo huwa zimeanza kubadili rangi.
• Kama yanapatikana, tumia madawa ya kibayolojia kama vile Aflasafe (aina ya kuvu ambaye hukinzana na yule anayetoa sumu kuvu).
• Tumia madawa yaliyodhibitishwa kuondoa sumu kuvu wakati wa usindikaji (utengenezaji) wa vyakula vya binadamu na vile vya wanyama.
No comments: