Uongozi wa klabu ya soka ya Simba umelitaka Bunge la Tanzania kupitia upya na kuifanyia marekebisho sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2016 ili kudhibiti watu wanaotumia mitandao ya kijamii kusambaza taarifa za uzushi.
Ombi hilo limetolewa jijini Mwanza na mkuu wa habari na mawasiliano wa klabu hiyo klabu hiyo, Haji Manara na kukanusha taarifa za uongozi wa klabu hiyo kudaiwa kutaka kumfukuza kocha wao mkuu mkenya, Joseph Omog.
Manara ambaye ameonekana kukerwa na taarifa za kwenye mitandao kuhusu kufukuzwa kwa kocha wao Joseph Omog kwa kutumia ‘Simba App’ ya kughushi, amesema kwa kiasi kikubwa taarifa hizo zimekuwa zikiathiri tasnia ya michezo pamoja na kuvuruga mustakabli wa klabu yao.
Ameitaka serikali itumie sheria hiyo ya makosa ya mitandaoni kuwadhibiti wanaotumia vibaya mitandao hiyo na kushauri kwamba kama sheria hiyo haina meno, ipelekwe bungeni ili ifanyiwe marekebisho.
Akiweka wazi msimamo wa klabu kuhusu kocha Omog, Manara amesema kocha huyo ni muhimu sana kwa klabu ya Simba kutokana na rekodi zake, akitolea mfano mechi alizokutana na Yanga.
“Katika mechi nne ambazo Simba imekutana na Yanga, Omog ameipiga Yanga mechi tatu. Kwa sasa Simba inamuhitaji Omog kuliko Omog anavyoihitaji Simba,” amesema Manara.
Akielezea hali ya timu yake kuelekea mchezo wao wa Jumamosi hii dhidi ya Stand United kwenye Dimba la CCM Kambarage mjini Shinyanga, Manara amesema kikosi hicho katika hali nzuri na kimejipanga kuchukua pointi tatu katika mchezo huo.
Related posts
Hii Hapa Taarifa Kutoka Simba Sc 27.09.2017
Reviewed by Informalblogsport
on
22:59
Rating: 5
No comments: